Chanzo, dalili, tiba na Madhara ya ugonjwa wa vionda vya tumbo (PUD)
Ugonjwa wa vidonda vya tumbo hutokea iwapo kidonda cha ukubwa wa angalau wa nusu sentimita kitatokea kwenye sehemu yeyote ya ukuta wa tumbo au utumbo wa binadamu.
Kwa kawaida tatizo hili huleta maumivu makali sana ya tumbo ingawa si lazima kila maumivu ayapatayo mgonjwa husababishwa na vidonda vya tumbo.
Tafiti zimeonesha kwamba karibu asilimia 70 mpaka 90 ya vidonda vya tumbo husababishwa na aina ya vimelea vya bakteria wajulikanao kama Helicobacter pylori. Aidha matumizi ya baadhi ya dawa za kutuliza maumivu za jamii ya Non Steroid Anti-inflamatory Drugs kama aspirin au diclofenac huweza kusababisha au kuongeza uwezekano wa kupata ugonjwa huu.
Kuna dhana iliyozoeleka kuwa vidonda vya tumbo huathiri zaidi mfuko wa kuhifadhia chakula yaani tumbo (stomach). Dhana hii si kweli kwani sehemu inayoathiriwa zaidi na tatizo hili ni sehemu ya kwanza ya utumbo mdogo ijulikanayo kama duodenum.
Makundi ya PUD
Kuna makundi makuu yafuatayo ya ugonjwa huu
- Vidonda vinavyotokea kwenye mfuko wa kuhifadhia chakula yaani tumbo (Gastric ulcers)
- Vidonda vinavyotokea kwenye sehemu ya kwanza ya utumbo mdogo (Duodenal Ulcers)
- Vidonda vinavyotokea kwenye koo (Oesophageal ulcers)
- Vidonda vijulikanavyo kama Merckel’s Diverticulum ulcers.
Visababishi vya PUD
Vidonda vya tumbo husababishwa na
Maambukizi ya bakteria aina ya Helicobacter pylori
Imeonekana kuwa zaidi ya asilimia 50 ya watu duniani wana vimelea hivi katika utumbo. Aidha, miongoni mwao, karibu asilimia 80 huwa hawaoneshi dalili yeyote ya kuugua ugonjwa wa vidonda vya tumbo.Aina hii ya vimelea vya bakteria husababisha karibu asilimia 60 ya vidonda vinavyotokea kwenye tumbo (gastric ulcers) na zaidi ya asilimia 90 ya duodenal ulcers.
Hali hii husababishwa zaidi na kushindwa kwa mfumo wa kinga mwilini kuwaua na kuwaondoa kabisa vimelea hawa ndani ya mwili. Matokeo ya kushindwa huku husababisha kuwepo kwa maambukizi ya kudumu katika kuta za tumbo (chronic active gastritis), maambukizi ambayo huharibu mfumo na uwezo wa kuta za tumbo kutunza homoni/kichocheo aina ya Gastrin, ambacho ni muhimu katika kuhakikisha mazingira ya tumbo yanakuwa na kiwango salama cha tindikali.
Kwa kawaida, kazi ya gastrin ni kuchochea utolewaji wa tindikali (gastric acid) kutoka kwenye seli za ukuta wa tumbo zijulikanazo kama Parietal cells. Iwapo bakteria hawa watashambulia na kuharibu ukuta wa tumbo, mfumo wa gastrin pia uharibika, na hivyo kusababisha gastrin kuzalishwa kwa wingi hali ambayo pia huchochea uzalishaji wa gastric acid kwa wingi. Matokeo ya kuzalishwa kwa wingi kwa tindikali hii hupelekea kuchubuka kwa ukuta wa tumbo na hivyo kusababisha vidonda vya tumbo.
Matumizi ya muda mrefu ya dawa za kuondoa maumivu za kundi la NSAIDs
Ukuta wa utumbo hujilinda na madhara yatokanayo na tindikali ya utumbo (gastric acid) kwa kuwa na utando laini (mucus) ambao hutolewa na vichocheo vijulikavyo kama Prostaglandins. Dawa hizi za kundi la NSAIDs huharibu mfumo wa kutengeza vichocheo hivi yaani prostaglandins na hivyo kufanya kuta za tumbo kukosa utando wa kuzilinda na mashambulizi ya tindikali hali ambayo hupelekea kutokea kwa vidonda vya tumbo.
Uvutaji wa sigara
Uvutaji sigara sambamba na maambukizi ya bakteria aina ya Helicobacter pylori huongeza madhara ya ugonjwa wa vidonda vya tumbo. Ifahamike tu kuwa uvutaji sigara pekee hausababishi vidonda vya tumbo.
Vyakula au viungo vya chakula vyenye uchachu
Kinyume na dhana iliyozoeleka miongoni mwa watu wengi, baadhi ya vyakula vyenye uchachu na upilipili kama vile pilipili, ndimu, limao na masala havina uhusiano na uwezekano wa kupata vidonda vya tumbo.
Watu walio katika kundi la damu la O
Imeonekana pia kwamba kundi la damu lijulikanalo kama blood group O, halina uhusiano wa kusababisha vidonda vya tumbo.
Unywaji wa pombe
Unywaji wa pombe pekee hausababishi vidonda vya tumbo. Hata hivyo, unywaji wa pombe sambamba na maambukizi ya vimelea vya Helicobacter pylori huongeza madhara ya ugonjwa wa vidonda vya tumbo.
Vitu vingine
Vitu vinavyohusishwa na uongezaji wa madhara ya vidonda vya tumbo ni pamoja na upasuaji wa tumbo (major abdominal surgeries), kuungua kwa moto (burns), ugonjwa wa figo; na kubadilishwa kwa viungo vya mwili kama figo au ini.
Dalili au viashiria vya PUD
Maumivu makali au kiungulia maeneo ya chembe moyo (epigastic pains): Maumivu juu kidogo ya tumbo mara nyingi huendana na muda wa kula chakula. Mtu mwenye vidonda kwenye tumbo (gastric ulcers) hupata maumivu makali sana kipindi anapokula au mara tu baada ya kumaliza kula wakati aliye na vidonda kwenye sehemu ya kwanza ya utumbo mdogo (duodenal ulcers) hupata maumivu makali anapokuwa na njaa na hupata nafuu pindi anapokula.
- Kuvimbiwa au tumbo kujaa gesi. Hali hii pia yaweza kuendana na kubeua au kujamba mara kwa mara.
- Kucheua na kuongezeka kwa mate yanayoshuka tumboni baada ya kucheua.
- Kichefuchefu na kutapika
- Kupoteza hamu ya kula na kupungua uzito
- Kutapika damu
- Kupata haja kubwa ya rangi nyeusi au kahawia yenye harufu mbaya sana. Hii humaanisha mgonjwa anapata haja kubwa au choo kilichochanganyika na damu kwa mbali
Uwepo wa dalili kama kiungulia cha muda mrefu, kucheua na kutapika baada ya kula na historia ya kutumia dawa za kupunguza maumivu (NSAIDs) kwa muda muda mrefu bila kufuata ushauri wa daktari ni ishara tosha ya kumfanya mgonjwa kumuona daktari kumpima na kumfanyia uchunguzi ili kujiridhisha kuwa hana tatizo la vidonda vya tumbo.
Vipimo vya kutambua Ugonjwa wa vidonda vya tumbo
Vipimo vinavyotumika katika kutambua tatizo la vidonda vya tumbo ni pamoja na
Vipimo vya kuangalia ndani ya utumbo ambavyo ni pamoja na
- Kipimo cha oesophagogastroduodenoscopy (EGD) au Upper GI endoscopy au gastroscopy. Kwa kutumia kipimo hiki, daktari huangalia moja kwa moja ndani ya utumbo wa mgonjwa kuona sehemu iliyo na vidonda pamoja na ukubwa wa tatizo lake. Aidha vipimo hivi humuwezesha daktari kuchukua sehemu ya utumbo iliyoathiriwa kwa ajili ya kuchunguza zaidi maabara ili kutambua uwepo wa vidonda au tatizo jingine linalomsumbua mgonjwa tofauti na vidonda vya tumbo.
- Kipimo kingine kijulikanacho kama Barium meal kina uwezo pia wa kuthibitisha uwepo wa ugonjwa wa vidonda vya tumbo.
Vipimo vya kutambua uwepo wa uambukizi wa bakteria aina ya Helicobacter pylori kama
- Kipimo kiitwacho Urea breath test
- Kipimo cha kuotesha kinyama kilichochukuliwa kutoka katika kipimo cha OGD (culture from an OGD biopsy specimen).
- Kipimo kinachoitwa Rapid Urease Test ambacho hufanywa kwa kutumia kinyama kilichochukuliwa kutoka kwenye utumbo wakati wa kufanya OGD. Kipimo hiki huangalia tabia ya vimelea hawa wa H. pylori.
- Kipimo cha damu kwa ajili ya kutambua kiwango cha maambukizi ya vimelea wa H. pylori (antibody levels).
- Kipimo cha haja kubwa kwa ajili ya kutambua kama bakteria wapo hai au wamekufa (stool antigen test). Kipimo hiki ni cha uhakika zaidi na nafuu kuliko kipimo cha Urea Breath Test.
- Kipimo cha kimaabara cha kuchunguza kinyama kilichochukuliwa wakati wa kipimo cha OGD.
Vipimo vingine maalum vya kitaalamu zaidi kama
- Kiwango cha homoni ya gastrin katika damu
- Kipimo cha kuangalia uzalishaji wa homoni ya secretin ambayo uhusika katika uchocheaji wa homoni ya gastrin
- Kupima kiwango cha tindikali inayozalishwa katika tumbo.
Hata hivyo vipimo hivi ni vya gharama zaidi na ni aghalabu hutumika mara kwa mara.
Matibabu ya Ugonjwa wa vidonda vya tumbo
Habari nzuri ni kuwa ugonjwa huu wa vidonda vya tumbo unatibika. Hata hivyo tabia ya baadhi ya wagonjwa wengi kuacha kumalizia dawa au kutumia dawa chini ya kiwango tofauti na walivyoshauriwa na madaktari husababisha kujirudia kwa tatizo au kufanya tatizo kuwa sugu zaidi.
Iwapo itagundulika uwepo wa H. pylori tiba inayotumika ni kuchanganya dawa za antibayotic (antibiotic) za aina tofauti kama Amoxicillin, Tetracycline, Clarithromycin au Metronidazole na dawa zenye uwezo wa kupunguza uzalishaji wa tindikali kwa wingi au kwa kitaalamu Proton Pump Inhibitors (PPI). Wakati mwingine daktari anaweza pia kuongeza dawa ya Bismuth Compound.
Kwa wagonjwa sugu, dawa za antibiotic za aina tatu tofauti zinaweza kutumika. Dawa hizi ni pamoja na Amoxicillin + Clarithromycin + Metronidazole ambazo hutumika sambamba na dawa yeyote moja kutoka kundi la PPI kama vile Omeprazole au Pantoprazole pamoja na Bismuth Compound.
Kwa mgonjwa wa kawaida ambaye si sugu tiba bora inayoshauriwa ni kuchanganya dawa za antibiotic za aina mbili kama Amoxycillin + Metronidazole sambamba na dawa yeyote moja ya jamii ya PPI kama Pantoprazole.
Iwapo hakuna ushahidi wa kuwepo kwa uambukizi wa bakteria, dawa yeyote moja ya jamii ya PPI yaweza kutumika kwa muda mrefu zaidi bila kuchanganya na antibiotic yeyote.
Kwa kawaida kitendo cha kutibu na kuwaondoa Helicobacter Pylori humaliza na kuponyesha kabisa vidonda vya tumbo.
Hata hivyo, inawezekana kabisa ugonjwa huu kujirudia tena, hali ambayo hulazimisha kurudiwa tena kwa matibabu kwa kutumia aina nyingine ya antibiotics.
Aidha msomaji, unashauriwa si vyema kwa mgonjwa kujitibu mwenyewe bila kufuata ushauri wa daktari ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea iwapo dawa hazitatumiwa inavyopaswa.
Ni kweli Maziwa ya ng’ombe yanaponyesha vidonda vya tumbo?
Kinyume na dhana iliyozoeleka ndani ya jamii, maziwa ya ng'ombe hayaponyeshi vidonda vya tumbo, bali huongeza madhara yatokanayo na ugonjwa huu. Hii ni kwa sababu, maziwa huwa na tabia ya kutengeneza aina fulani ya kinga au ukuta (protective coat) kwa vimelea vya Helicobacter Pylori ambayo huvikinga vimelea hivi dhidi ya mashambulizi ya dawa na hivyo kufanya dawa kushindwa kuwaua na kuwaondoa kabisa vimelea hivi.
Kinachotokea ni kuwa, maziwa huondoa tu kwa muda maumivu ya tumbo kwa kupunguza makali ya tindikali iliyopo tumboni. Pindi maziwa haya yanapoisha, maumivu hurejea tena na kuwa makali kama hapo awali.
Matibabu ya vidonda vya tumbo kwa njia ya upasuaji
Zipo aina nyingi ya upasuaji unaofanywa ili kutibu ugonjwa huu. Kuvuja damu ndani ya mwili kupitia vidonda vya tumbo ni sababu mojawapo ya kufanyiwa upasuaji kwa vile ni hatari sana hata kupelekea kifo iwapo mgonjwa hatapata tiba haraka
- Endoscopy: Ni njia inayotumika kutibu uvujaji wa damu unaotokana na vidonda vya tumbo. Aina hii ya tiba hutegemea sana aina na sehemu vilipo vidonda vya tumbo. Tiba hii yaweza kufanyika kwa kuchoma sehemu inayovuja damu ndani ya tumbo au utumbo kwa lengo la kusitisha uvujaji wa damu (cautery) au kwa kuvifunga vidonda kwa kutumia vifaa maalum (clippings). Aidha tiba hii ni nzuri na haina madhara yeyote yale.
- Madaktari wengi hupendelea upasuaji ujulikanao kitaalamu kama simple oversewing sambamba na tiba ya kuondoa bakteria. Aidha, mgonjwa pia hushauriwa kuacha matumizi ya dawa za NSAIDs kwa ajili ya kuondoa uwezekano wa damu kuendelea kutoka kwa vile kama ilivyoonekana hapo awali, matumizi ya dawa hizi huweza kusababisha uvujaji wa ndani kwa ndani ya mwili.
- Wagonjwa sugu, hufanyiwa baadhi ya upasuaji ambao huitaji utaalamu wa hali ya juu katika kuondoa neva na mishipa ya fahamu yenye kuhusika na uzalishaji wa tindikali katika tumbo.
Madhara ya ugonjwa wa vidonda vya tumbo
- Uvujaji wa damu ndani ya utumbo: Hali hii yaweza kusababishwa na vidonda kuenea hadi kwenye mishipa ya damu na hivyo kufanya damu kuanza kuvuja. Hali hii ni hatari sana na inahitaji tiba ya dharura.
- Vidonda vya tumbo huweza kusababisha tundu (kutoboka kwa ukuta wa tumbo) na kufanya vitu vilivyo ndani ya utumbo kutapakaa katika tumbo (abdomen) Hali hii huitwa peritonitis na ni hatari sana na inahitaji matibabu ya dharura. Aidha, kuenea huko kunaweza pia kuathiri tezi kongosho na kusababisha madhara katika tezi hiyo, ugonjwa unaojulikana kama pancreatitis.
- Vidonda vya tumbo vinaweza pia kuenea na kuathiri pia viungo vya jirani kama vile ini au kongosho (pancrease)
- Kuvimba kwa kuta za tumbo pamoja na makovu yanayosababishwa na vidonda hivi huweza kusababisha kuziba kwa njia ya kupitishia chakula kutoka kwenye tumbo (stomach) kwenda sehemu ya kwanza ya utumbo mdogo (duodenum) hali ambayo kitaalamu huitwa gastric outlet obstruction.
- Iwapo vidonda vya tumbo vimesababishwa na H. pylori, kuna uwezekano wa kati ya mara tatu hadi ya sita ya mgonjwa kupata kansa ya tumbo (stomach cancer).
No comments: