Header Ads

Maana Ya Magonjwa Nyemelezi Kwa Binadamu

Magonjwa nyemelezi ni yale ambayo hushambulia mwili wa binadamu pale uwezo wa kinga ya mwili kupigana na vimelea vya magonjwa unaposhuka.
Ni magonjwa ambayo katika hali ya kawaida hayategemewi kujitokeza kwa mtu mwenye kinga kamili ya mwili.
Kwa kawaida mwili wa binadamu yeyote umeumbwa na kinga ya mwili ya asili ambayo lengo lake kuu ni kuulinda mwili dhidi ya vimelea vya magonjwa.Inapotokea kimelea (vimelea) kuingia katika mwili wa binadamu kwa njia yoyote (kunywa au kula vimelea,kugusana na majimaji au ngozi ya mtu mwenye vimelea,au kupitia damu yenye vimelea n.k), mwili hutengeneza kingamwili (antibodies) ambazo hupigana na vimelea hivyo ili kuuweka mwili katika afya njema kama hapo awali.

Kushuka kwa kinga ya mwili hupelekea mwili kushindwa kupigana na vimelea vya magonjwa hivyo kusababisha kushambuliwa na magonjwa.Ifahamike kwamba baadhi ya vijidudu(microorganisms) pia hupatikana katika mwili wa binadamu bila madhara yoyote (normal flora) kama vile kwenye ngozi, mfumo wa chakula, ukeni, uumeni n.k Hata hivyo vijidudu hivi huweza kuwa chanzo cha magonjwa iwapo kinga ya mwili itashuka.
`

Vitu gani hupelekea kushuka kwa kinga ya mwili?

Sababu mojawapo kubwa ya kushuka kwa kinga ya mwili haswa katika nchi zilizopo chini ya jangwa la Sahara ni Ukimwi/VVU.Hata hivyo ieleweke kwmba si kila mtu mwenye upungufu wa kinga mwilini ana VVU.

Kuna sababu nyingine nyingi ambazo husababisha kwa njia moja au nyingine kushuka kwa kinga ya mwili.Zifuatazo ni baadhi tu ya sababu hizo;

Utapiamlo, Kuugua mara kwa mara,Sababu za kijenetiki (kurithi),Madhara kwenye ngozi,Msongo wa mawazo na Ujauzito. Madawa ya Kutibu saratani, Matumizi ya muda mrefu ya antibayotiki (antibiotics),steroidi (steroids) na madawa ya kushusha kinga mwilini (immunosuppressant drugs)) ambayo hutumika wakati wa kupandikiza viungo mwilini kama figo n.k

Magonjwa nyemelezi husababishwa na vijidudu mbalimbali kama bacteria,virusi,fangasi na bakteria.

Bakteria

Baadhi ya magonjwa yasababishwayo na bakteria ni kama yafuatayo;

Kifua Kikuu (TB)
Ugonjwa huu husababishwa na kimelea kiitwacho Mycobacterium tuberculosis ambacho ni moja katika kundi la Mycobacterium Avium Complex (MAC).Kushuka kwa kinga ya mwili hupelekea kulipuka kwa vimelea vya kifua kikuu ambavyo hupatikana, pamoja na viungo vingine, zaidi kwenye mapafu.
Dalili za kifua kikuu ni pamoja na kikohozi na homa (haswa nyakati za usiku) kwa zaidi ya wiki mbili.Kutokwa jasho usiku (mara nyingi jasho huwa jingi mpaka kulowesha shuka),kupungua uzito (zaidi ya kilo moja na nusu ndani ya mwezi), Kichomi na kukohoa damu.
Ugonjwa huu pia huweza kupelekea kupata homa ya uti wa mgongo(meningitis) ambayo huambata na dalili kama kuumwa kichwa, kichefu chefu na kutapika ikifutiwa na kuongezeka kwa joto la mwili na maumivu na kukaza kwa shingo.

Nimonia (Pneumonia)
Huu ni ugonjwa ambao kwa kiasi kikubwa huathiri mfumo wa hewa na haswa mapafu.Baadhi ya vimelea viletavyo nimonia ni kama Pneumococcus ,Haemopilus influenza, Mycoplasma (haswa kwa watoto) pia Klebsiella, Staphylococcus aureus, Pseudomonas aeuroginosa (kwa wagonjwa waliolazwa mahospitalini) na wengineo.
Ugonjwa huu huanza ghafla na dalili zake ni kama homa kali, kikohozi, maumivu wakati wa kupumua, baridi na kutetemeka.

Ugonjwa wa Ngozi
Huu husababishwa na vimelea vya Staphylococcus aureus.Vimelea hivi huishi katika mwili wa binadamu (kwenye ngozi ya kichwa na kinena (groins) na kwapani) bila madhara.Pia hupatikana kooni na katika utumbo mpana na mkojo.
Vimelea vya Staphylococcus husambaa kwenda sehemu nyingine ya mwili kutoka kwenye usaha, mgusano na ngozi ya mwenye maradhi, kutumia taulo, matandiko,vifaa vya mtu aliyeathirika n.k

Dalili zake ni pamoja na chunusi, majipu, kubabuka kwa ngozi na magamba magamba katika ngozi.


Magonjwa ya Virusi


Magonjwa yasababishwayo na virusi ni kama;

Ugonjwa wa Malengelenge
Husababishwa na virusi vya Herpes Simplex.Hivi vimegawanyika katika Herpes Simplex Virus-1 (HSV-1) na Herpes Simplex-2 (HSV-2).Virusi vya HSV-1 vyaweza ambukizwa kupitia ngozi laini (mucous membranes) za mwili na kubusiana.Huweza kusababisha mwasho kwenye midomo,ulimi,fizi za meno au kingo za juu za kinywa (buccal mucosa).Kwa upande wa virusi vya HSV-2 hivi huweza kusababisha michubuko na maumivu kwenye uume,uke na njia ya haja kubwa.

Katika kiwango cha juu cha ugonjwa viungo vingine vya mwili kama macho, njia ya chakula, mfumo wa fahamu na na njia za mfumo wa hewa huathirika.

Dalli balimbali za ugonjwa huu ni malengelenge (blisters), mwasho na muunguzo.Kushindwa kumeza au kupata maumivu wakati wa kumeza (haswa chakula),tezi kuvimba na maumivu wakati wa haja kubwa au ndogo.

Mkanda wa jeshi
Husababishwa na kirusi kiitwacho Varicella Zoster (VSV).Mara nyingi hutokana na kuamshwa kwa ugonjwa ambao ulikuwepo mwilini hapo Awali (reactivation of an earlier infection).Mbali ya kuathiri ‘uwanda’ (dermatome) moja au zaidi wa mishipa ya fahamu (neva),pia huweza kudhuru jicho (herpes zoster opthalmicus) na sikio (herpes zoster oticus).
Dalili zake ni maumivu makali katika ‘uwanda’ ulioathirika, homa, vipele, maumivu ya kichwa, uchovu na maumivu ya macho kutokana na mwanga (photophobia).

Maumivu ya Retina
Kwa lugha ya kitaalamu huitwa CMV Retinitis na husababishwa na kirusi kiitwacho Cytomegalovirus (CMV).Kirusi hiki, mbali ya kuathiri jicho na haswa retina, pia huathiri viungo vingine kama mapafu na kusababisha nimonia, utumbo mpana na mfumo wa fahamu ambako husababisha maumivu.

Dalili zake ni pamoja na kutoona vizuri, macho kuuma, kutokwa na machozi kwa wingi.Kutopata matibabu mapema huweza kusababisha upofu.Pia Huweza kuathiri viungo vingine na kusababiosha homa, nimonia, kichefuchefu, kuharisha na kupungua uzito.

Magonjwa yatokanayo na Fangasi

Fangasi pia huweza kujitokeza iwapo kinga ya mwili itashuka.

Kandidiasisi
Ugonjwa huu uliozoeleka pia hujulikana kwa kitaalamu kama Candidiasis.Kandidiasisi husababishwa na fangasi aitwaye Candida albicans ambaye huathiri kinywa, mfumo wa chakula,uke na mfumo wa hewa.Kandidiasisi katika uke huweza tokea kwa mwanamke mwenye afya asiye na VVU.

Dalili za Kandidiasisi katika kinywa ni pamoja na kubadilika kwa ladha,maumivu kwenye ulimi,utando mweupe kwenye ulimi na kingo za juu za kinywa (buccal mucosa),kushindwa kumeza,maumivu wakati wa kumeza chakula ikiwa fangasi imesambaa sana. Pia mwasho na maumivu ukeni pamoja na kutokwa na majimaji meupe ukeni.

Homa ya Uti wa mgongo
Homa ya utiw amgongo au Meningitis kwa kitaalamu husababishwa na fangasi aitwaye Cryptococcal neoformans.Uti wa mgongo utokanao na aina hii ya fangasi huweza kusababisha kifo usipotibiwa.Aina hii ya fangasi ambayo huathiri zaidi ubongo na uti wa mgongo, hutokana na kuvuta hewa yenye vumbi litokanalo na ndege lenye vimelea vya ugonjwa.
Baadhi ya dalili zake ni homa, kutoona vizuri,macho kuuma kutokana na mwanga,kuchanganyikiwa akili,maumivu ya kichwa ka kukakamaa na kuuma kwa shingo.

Histoplasmosisi
Aina hi ya fangasi hutokana na vimelea vya Histoplasma capsulatum.Fangasi huyu huathiri mapafu pamoja na viungo vingine.Dalili zake ni homa,uchovu,kupungua uzito na kupumua kwa shida.Pia kukohoa na kuvimba kwa tezi kwaweza kutokea.


Nimonia

Kama bakteria na fangasi pia huweza kusababisha nimonia ijulikanayo kwa kitaalamu kama Pneoumocystis Pneumonia (PCP).Vimelea vya Pneumocystis jiroveci (awali vilijulikana kama Pneuomocystis carinii) huathiri mfumo wa hewa.Fangasi huyu pia huweza kuathiri viungo vingine kama ini,wengu (spleen) na figo katika baadhi ya wagonjwa.
Dalili zake ni kikohozi kikavu,kifua kubana,kupumua kwa shida,homa,kuishiwa pumzi na kutokwa jasho nyakati za usiku.

Magonjwa yatokanayo na Protozoa

Toksoplasmosisi ya Ubongo
Cerebral toxoplasmosis, kama ujulikanavyo kitaalamu,hutokana na kuamshwa kwa ugonjwa wa awali kutokana na vimelea vya Toxoplasma gondii (kimelea kiwezacho kuishi ndani ya seli kinachoathiri ndege,wanyama na binadamu).Kimelea hiki kiathiricho zaidi mfumo wa fahamu,hupatikana kwenye nyama isiyopikwa vizuri na mavi ya paka.Huathiri zaidi ubongo na kusababisha maumivu ya kichwa,kuchanganyikiwa,udhaifu wa viungo,homa,kupoteza fahamu,kupooza na kifafa.

Kriptosporidiosisi
Huu ni ugonjwa utokanao na vimelea vya Cryptosporidium.Huathiri zaidi mfumo wa chakula na hutokana na kutumia kwa maji au chakula vilivyoathirika na vimelea vya ugonjwa huu.Dalili zake ni kuharisha sana kiasi cha kusababisha kupungukiwa na maji mwilini (dehydration),maumivu wakati wa haja kubwa, kichefuchefu na kutapika.Wagonjwa wa aina hii huwa na joto la mwili la kawaida.

Matibabu na Ushauri

Aina ya matibabu hutegemea na aina ya ugonjwa na mtu, pia kutokana na kuwepo kwa Ukimwi/VVU hutegemea kiwango cha seli za CD4 mwilini.Iwapo una dalili kati ya zilizotajwa hapo juu ni vyema kumona daktari kwa uchunguzi zaidi.
Ni vyema kuzingatia kuwepo kwa dalili zilizotajwa hapo juu hakumanishi kuwa muathirika ana VVU na si kila mwenye VVU huwa na dalili hizo.Pia kujitokeza kwa dalili kunaweza kutofautiana kati ya mtu na mtu.Hata hivyo ni vyema kupima afya yako kila mara haswa VVU ili kujua chanzo cha kupungua kwa Kinga ya mwili ambayo huweza kupelekea kupata magonjwa nyemelezi

No comments:

Powered by Blogger.