Header Ads

Msongo wa mawazo unaweza kuzuia usipate ujauzito

Msongo wa mawazo unaweza kuzuia usipate ujauzito

Wakati ukitafuta ujauzito mara nyingi unapata ushauri wa kila namna toka kwa watu wengi unaowafahamu.
Moja ya ushauri utaupata ni kujitahidi kutokuwa na msongo wa mawazo (stress). Huu ni moja ya ushauri wa mhimu sana kuuzingatia ingawa hujuwi ni kwanini unaambiwa hivyo na matokeo yake ni nini kama hutazingatia hilo.
Moja ya sababu kubwa kwanini unaambiwa usiwe na stress wakati unatafuta ujauzito ni kuwa stress inaharibu na kuvuruga mfumo wako wote wa uzazi na kinachovurugwa cha kwanza kabisa ni mfumo wako wa homoni.
Ili kupata ujauzito, homoni ya uzazi ijulikanayo kama ‘progesterone’ ambayo huzalishwa kwenye ovari lazima iwe inafanya kazi vizuri na kwa usawa unaohitajika.
Usawa wa homoni hii ya Progesterone ni wa mhimu kama unataka kupata ujauzito bila vikwazo.
Mwanamke anapokuwa kwenye siku za kupata ujauzito joto la mwili wake huongezeka hasa sehemu yake ya chini kuanzia tumboni.
Wakati huo huo joto linaongezeka pia katika homoni ya uzazi progesterone. Ikiwa joto litashuka katika progesterone inamaana tayari mwanamke ameshaingia kwenye siku zake au ujauzito umetoka.
Mwili unapokuwa umesongwa na mawazo mengi (stress) kwa muda mrefu hutengeneza homoni nyingine iitwayo Cortisol ili kuuwezesha mwili kuhimiri hali hiyo ya mfadhaiko.
Sasa hii homoni Cortisol imeundwa kwa homoni kama zile zile zilizomo kwenye homoni ya uzazi progesterone na wakati mwili unapokumbwa na mawazo mengi homoni hizi zote mbili zinaelekezwa kwenye kuushughurikia huo msongo wako wa mawazo na kama matokeo yake hakuna chochote kinachoelekezwa kushughurika na mambo ya uzazi!
Kwahiyo shida inaanzia hapo.
Na ndiyo maana huwa unasikia watu wanasema unapocheka mara kwa mara siku zako za kuishi zinaongezeka.
Ni kwa sababu unapokuwa na furaha kinga yako ya mwili inaongezeka na mambo mengi maishani mwako utaona yanakunyookea kuliko unapokuwa mtu wa kununa nuna tu kila wakati.
Wanandoa wengi ninaokutana nao kwa shida za uzazi ninaowashauri kwamba wakati wakisubiri kurekebisha athari kwenye afya zao za uzazi wajitahidi kadri iwezekanavyo wasiwe na mawazo mawazo wengi wao wanafanikiwa kupata ujauzito ndani ya muda mfupi.
Kuna mtu anauliza inawezekanaje kuondoa hii hali ya msongo wa mawazo na nina tatizo kama hili miaka kadhaa sipati ujauzito?
Sikia, inawezekana na ni rahisi lakini pia inaweza isiwezekane na ikawa ngumu sana kwako kama utaamua iwe hivyo. Ndiyo mwamuzi wa mwisho ni wewe.
Ndoa siyo kuwa tu na watoto. Yaani kinachofanya ndoa iwepo siyo watoto. Wala dhumuni hasa la kuoana siyo watoto. Wala watoto siyo sababu ya kudumu kwa ndoa.
Na tena naweza kuongeza kuwa hata maisha siyo kuoa au kuolewa tu. Kuoa au kuolewa siyo tiketi ya kwenda mbinguni. Pia kuoa au kuolewa ni jambo la hapa hapa duniani tungali tukiwa hai, mbinguni kuoa au kuolewa haipo (Mathayo 22 : 30).
Dunia tayari ina watu weengi sana na hatuelewi itakuwaje miaka 1000 toka sasa sababu ndani ya miaka 100 tu iliyopita idadi ya watu imeongezeka mara 3 zaidi.
Nchi kama China kwa sasa huruhusiwi kuzaa watoto zaidi ya wawili, ni sheria ya nchi kabisa, huruhusiwi kuwa na watoto zaidi ya wawili.
Heshima na kujaliana ndiyo mambo mawili mhimu zaidi katika ndoa
Sasa unaanzaje?
Mkabidhi Mungu kila kilicho chako, jikabidhi na wewe mwenyewe kwa Mungu.
Mwambie Mungu mimi nahisi (ndiyo sema nahisi na siyo NINA ..).
Mwambie Mungu nahisi nina tatizo la kutokupata ujauzito, hivyo liangalie hilo na unipe majibu kadri ya mapenzi yako kwangu. Basi halafu acha hilo jambo endelea na maisha mengine.
Relax
Ni mhimu jambo hili la umhimu wa kutokuwa na mawazo wakati unatafuta ujauzito lifahamike kwa wanandoa wote wawili.
Msongo wa mawazo peke yake (stress) unasemwa na wataalamu mbalimbali wa afya kwamba unaweza kukusababishia magonjwa mengine mwilini zaidi ya 50 ikiwemo kuharibu mfumo wa homoni, kushusha kinga ya mwili na mengine mengi bila idadi.
Kwa bahati nzuri kuna namna nzuri za kuondoa tatizo la msongo wa mawazo na hivyo kuujulisha mwili wako kwamba upo tayari kushika ujauzito.
Kuwa bize na kazi, fanya mazoezi ya viungo kila siku, kunywa maji mengi kila siku, usikae mpweke, tumia muda mwingi kusali, shiriki tendo la ndoa mara kwa mara, kula chakula sahihi (hasa vyakula vyenye madini ya magnesium), epuka vilevi, epuka ugomvi mdogo mdogo wa kijinga nk
Kama mmekaa zaidi ya miaka mitano na mnaona hakuna dalili kabisa za kupata mtoto basi nendeni kituo cha watoto yatima ombeni mtoto mmoja mkae naye, mmtunze na kumsomesha kama vile ni wakwenu.
Tuna vituo vingi sana Tanzania vya watoto yatima, unaweza kwenda huko na ukapewa mtoto. Utakuwa umetoa sadaka kwa Mungu na atakubariki kwa ajili hiyo.
Kuna mtu anasema sasa mimi nina mali nyingi kama nakufa atarithi nani kama sina mtoto. Pole sana ndugu. Pole.
Nani amekutuma huku duniani kuja kuandaa mali za watoto wako?.
Hizi mali zote ni za Mungu ulizikuta na utaziacha na ni mali kwa ajili ya watu wote akiwemo na mwanao. Kila mtu akizaliwa Mungu humuwekea vipaji vyake vimfanikishe katika maisha yake.
Sasa inapotokea mtoto anazaliwa tayari ana nyumba, tayari ana gari, tayari ana kampuni, tayari ana hela bank kunamfanya mtoto huyu kuwa zezeta, anakuwa hana akili wala busara. Kunamharibia uwezo wa ubongo wake wa kutumika kwa ajili ya jamii yake inayomzunguka.
Zawadi pekee unaweza kumuandalia mtoto ni kumlipia tu ada ya shule.
Kwahiyo kama una mali na huna mtoto ukifa tupo wajomba zako tutarithi. Na kama unaona shida sana sisi turithi mali zako unaweza kuandika waraka kwamba nikifa mali zangu zipelekwe kituo cha watoto yatima.
Kuna ndugu wengine ndiyo wanaleta misongo ya mawazo kwenye ndoa za watu eti utasikia mbona huyo mkeo hazai? Anakula bure tu?.
Kaa mbali na watu wenye mawazo mgando kama hao wanaosema mbona mkeo hazai. Waambie atazaa wakati ukifika na hatukuoana ili kuzaa.
Mme ndiyo unahitajika kuwa na msimamo usioyumba na ndiyo uongoze maombi kila siku nyumbani na mwambie mkeo tutaishi, tutafurahi hata kama hatupati mtoto na muda ukienda sana tutaenda kituo cha watoto yatima tuchukuwe mtoto wetu tuendelee na mambo yetu mengine.
Uwezo wako wa kubeba ujauzito unaongezeka mara mbili zaidi unapokuwa huna msongo wa mawazo.
Ndoa siyo kuwa na watoto tu.

No comments:

Powered by Blogger.