Header Ads

Msongo Wa Mawazo Wakati Wa Ujauzito Husababisha Ulemavu Kwa Mtoto

 Ripoti ya watafiti hao inazidi kuthibitisha matokeo ya tafiti  zilizopita kuwa mama mwenye msongo wa mawazo wakati wa ujauzito kutokana na mambo kama kufukuzwa au kuachishwa kazi,kutengana na mwenza wake au kufiwa ana hatari ya kuzaa mtoto mwenye ulemavu kama vile midomo sungura (cleft lip na cleft palate) au matatizo kwenye uti wa mgongo (spina bifida).
Jopo la watafiti wa kidenmark likiongozwa na Dr Dorthe Hansen walifanya uchunguzi ili kuthibiitisha ukweli na uhakika wa  dhana hii.


Wakitumia rikodi za taarifa za kitabibu za kipindi cha miaka 12 kutoka 1980 mpaka 1992 kutoka masjala ya Taifa ya kitabibu,  watafiti hao waliweza kuwatambua wajawazito wote waliokumbwa na matatizo makubwa ya kimaisha wakati wa ujauzito na hata miezi 16 kabla ya kupata ujauzito. Matatizo makubwa ya kimaisha yaliyochunguzwa yalikuwa kukumbwa na msiba wa ndugu au jamaa wa karibu, ndugu au jamaa wa karibu kulazwa hospitali kwa mara ya kwanza baada ya kugundulika kuwa na kansa ya aina yeyote au ndugu au jamaa wa karibu kupatwa na ugonjwa wa mshtuko wa moyo. Mambo haya yalichunguzwa kwa kigezo kuwa, mjamzito yeyote aliyewahi kukumbana nayo ana hatari kubwa ya kuwa katika msongo wa mawazo bila kujali tabia yake, kama ana watu wa kumfariji au uwezo wake wa kukabiliana nayo.

Jopo hilo lilichunguza maendeleo ya mimba kwa wajawazito 3,560 ambao walikumbana na matukio hayo kwa kulinganisha na  wajawazito wengine 20,299 ambao hawakukumbana na hali yeyote ambayo ingewasababishia kupata msongo wa mawazo wakati waujauzito.



Matokeo ya uchunguzi wao yalionesha kuwa ulemavu na hitilafu za viungo kwa watoto waliozaliwa ulikuwa mara mbili miongoni mwa  kundi la wajawazito waliokumbwa na msongo mkali wa mawazo ikilinganishwa na kundi la kinamama ambao hawakuwa na hali hiyo.

Kadhalika ilionekana kuwa wanawake waliowahi kukumbwa na hali kama hiyo katika ujauzito mbili mfululizo za nyuma walikuwa katika hatari kubwa zaidi ya kuzaa watoto wenye ulemavu wa viungo tofauti na wale waliowahi kupatwa na hali hiyo mara moja tu au wale ambao hawakupatwa kabisa.

Ilionekana pia kuwa tukio lililoongeza uwezekano wa mtoto kuzaliwa akiwa na ulemavu wa viungo ilikuwa ni iwapo mjamzito atafiwa na mtoto wake mwingine mkubwa wakati akiwa katika miezi mitatu ya mwanzo wa ujauzito wake huu wa sasa. Hatari ya kuzaa mtoto mlemavu iliongezeka iwapo kifo cha mtoto huyo mkubwa kingetokea bila kutarajiwa kwa mfano kwa ajali.

Watafiti wanasema kwamba, msongo mkali wa mawazo huchangia kuathiri uumbaji wa mtoto aliye tumboni kwa kusisimua uzalishaji  wa homoni ya cortisone. Homoni hii husababisha ongezeko la kiwango cha sukari katika damu na upungufu wa usambazaji wa hewa safi ya oksijeni kwa mtoto, mambo ambayo husababisha kutokea kwa hitilafu katika uumbaji wa viungo vya mtoto hatimaye kusababisha ulemavu wa viungo vya mtoto.

Uwezekano mwingine ni kuwa msongo mkali wa mawazo humchochea mama mjamzito kutumia zaidi vileo vyenye alcohol na pia kula  lishe duni hali ambayo huongeza madhara zaidi kwa kiumbe kilicho tumboni.

Hata hivyo Professor Peter Hepper wa Chuo Kikuu cha Queen's cha Belfast, anasema hakushangazwa na mtokeo ya utafiti huo.

Anasema kuwa, "tunafahamu msongo wa mawazo husababisha mabadiliko ya kifiziolojia katika mfumo wa mwili wa mjamzito, na hivyo hakuna sababu kwanini mabadiliko hayo yasimfikie pia mtoto aliye tumboni kupitia kondo la nyuma na kumuathiri. Matokeo haya yanazidi kuthibitisha kile tulichokuwa tukikifahamu tangu awali kuwa msongo wa mawazo wa muda mrefu kwa mwanamke una madhara makubwa kwa mendeleo ya uumbaji wa mtoto aliye tumboni na hivyo basi hakuna budi kufanyike kila njia kuwasaidia wajawazito walio katika hali hii ili waweze kujifungua watoto walio na afya njema na salama."

No comments:

Powered by Blogger.