Header Ads

Matumizi Ya Dawa Wakati Wa Ujauzito

Ujauzito ni kipindi muhimu sana katika maendeleo na ukuaji wa mtoto tumboni mwa mama. Maendeleo na ukuaji huu unaweza kuathiriwa na vitu mbalimbali ikiwemo baadhi ya dawa zinazotumika wakati wa ujauzito.



Mjamzito anapokunywa dawa, dawa hunyonywa na kuingia kwenye damu ambapo huweza kuingia kwa mtoto kupitia kondo la uzazi. Baadhi ya dawa zinaweza kuleta madhara kwa mtoto tumboni ambayo yataathiri ukuaji wake. Kwa hiyo ni muhimu sana kuwa mwangalifu na dawa unazotumia wakati wa ujauzito. Ikumbukwe si dawa zote zitaathiri ukuaji wa mtoto.

Usalama Wa Dawa

Dawa hufanyiwa uchunguzi wa usalama wake wakati wa ujauzito. Utafiti huu huanza kufanyika kwa wanyama. Tafiti za kiepidemiolojia zinaweza kufanyika kuthibitisha usalama kwa binadamu wakati wa ujauzito. Hizi hufanyika kwa kutazama dawa wajawazito walizotumia na kama kuna madhara yaliyotokea kwa mtoto.

Pia usalama wa dawa hutofautiana kulingana na ukubwa wa mimba, kuna dawa ambazo si salama wakati wa miezi 3 ya kwanza lakini huweza kutumika miezi 4 na kuendelea ya mimba.

Mamlaka ya Dawa na Chakula Marekani (Foods and Drugs Authority – FDA) inagawanya dawa katika makundi 5 kutokana na usalama wake wakati wa ujauzito. Makundi haya ni:

  • Kundi A – Dawa hizi ni salama kutumia wakati wa ujauzito. Hazina madhara kwa mtoto tumboni wakati wa ujauzito na wakati wa kunyonyesha.
  • Kundi B – Salama kuitumia. Hakuna athari zinazoonekana kwa binadamu ingawa zinaweza kuwepo kwa wanyama wengine.
  • Kundi C – Zinaweza kuwa na madhara kwa mtoto. Tafiti kwa wanyama zinaonesha dawa hizi zinaweza kumdhuru mtoto tumboni, au hakuna ushahidi wa kutosha. Zinatumika pale ambapo faida ni muhimu ili kuokoa maisha ya mjamzito.
  • Kundi D – Kuna ushahidi wa madhara kwa mtoto tumboni. Itumike kuokoa maisha pale ambapo maisha ya mama yapo hatarini na hakuna dawa nyingine mbadala isipokuwa hiyo.
  • Kundi X – Hairuhusiwi kabisa kutumika wakati wa ujauzito.
Baadhi ya dawa ambazo ni salama wakati wa ujauzito ni Amoxicillin, Ampicillin, Clindamycin, Erythromycin, Penicillin na Nitrofurantoin.

Baadhi ya dawa zilizothibitishwa kuwa tishio kwa afya ya mtoto wakati wa ujauzito ni Streptomycin, Tetracycline, Cyclophosphamide, Cocaine, Methotrexate, Kanamycin, Ethanol, Valproic acid na Phenobarbital.

Madhara ya Dawa Wakati Wa Ujauzito kwa Mtoto

Dawa nyingi huleta madhara hasa miezi 3 ya mwanzo wa ujauzito. Hiki ni kipindi ambacho viungo mbalimbali vya mtoto huanza kutengenezwa, hivyo dawa pamoja na kemikali mbalimbali huweza kuathiri uumbaji wa viungo hivi na kuleta matatizo. Baadhi ya madhara yatokanayo na matumizi holela ya dawa wakati wa ujauzito ni:

Kupata maumbile yasiyo kawaida (malformations) ambayo yanaweza kuathiri kichwa, ubongo, moyo, figo, miguu,mikono na viungo vingine vya mwili.
Kutokua vizuri
Kufariki akiwa tumboni
Mtoto kudumaa tumboni
Mtoto kuzaliwa na uzito mdogo sana, njiti.
Mtoto kuzaliwa kabla ya wakati (premature birth)
Mimba kuharibika
Utindio wa ubongo

Mambo Ya Kuzingatia Kuhusu Dawa

Tumia dawa pale ambapo ni muhimu sana kutumika na ugonjwa umethibitishwa.
Mueleze daktari wako kuwa una ujauzito. Ni muhimu ajue ili usipewe dawa ambazo zinaweza kuwa na madhara kwa mtoto wako.
Kama unatarajia kuwa mjamzito, kuwa makini na matumizi ya dawa hasa wiki 2 baada ya kupata siku za hedhi kwani mimba inaweza kuwa imetunga lakini dalili hazijaanza bado.
Kama una tatizo au ugonjwa unaohitaji kunywa dawa kila siku, mueleze daktari wako palo unapofikiria kupata ujauzito.
Ni muhimu kuwa makini na matumizi ya dawa na kemikali mbalimbali sio tu wakati wa ujauzito bali hata kabla ya ujauzito na kipindi chote unachotarajia kuwa na mimba.
Kama italazimu kutumia dawa wakati wa ujauzito, basi hakikisha na daktari wako kuwa dawa ni salama na haitaleta madhara kwa mtoto tumboni mwako.

No comments:

Powered by Blogger.