Header Ads

Hiki ndio Chanzo cha Harufu Mbaya Mdomoni

Katika maisha ya kila siku yawezekana umewahi kukutana na mtu ambaye ukiwa karibu naye akiongea au kutoa pumzi kinywani au puani utasikia harufu mbaya.



Kwa kawaida mdomo na pua huweza kutoa pumzi nje ambayo huwa na harufu asilia ambayo haiwezi kumkera mtu mwingine, lakini mara zingine hali hiyo inaweza kujitokeza kutoa pumzi yenye harufu mbaya.

Watu wa karibu au wanaokutana na mwathirika wa hali hii wanaweza wakadhani kuwa ni mchafu mwenye tabia ya kutopiga mswaki au kutosafisha kinywa chake vizuri.

Pasipo kujua kuwa upo uwezekano mtu huyo akawa na tatizo linalojulikana kitabibu kama Halitosis,maana yake ni kutoa pumzi aidha kwa mdomoni au puani yenye harufu mbaya isiyo vumilika.

Mtu mwenye tatizo hili anaweza kukumbana na kunyanyapaliwa na wanajamii wanaomzunguka kiasi cha kuweza kumsababishia matatizo ya kisaikolojia.

Muathirika anaweza kupatwa na tatizo la woga/hofu iliyopitiliza anapokuwa kwenye kundi la watu, anaweza akajiondoa kutoka katika kundi hilo na kujitenga na vilevile, baadaye huweza kupata sonona (depression).

Tatizo hili linalowakumba asilimia 20 ya wajamii duniani, ni moja ya tatizo linalowafanya kufika katika huduma za afya kuwaona madaktari wa kinywa na meno.

Hufika kwa wataalam hawa wakidhani wana magonjwa ya kinywa ikiwamo mashimo katika meno, kulika kwa meno, kuoza kwa meno na magonjwa ya fizi.

Si wagonjwa wote wenye kutoa pumzi yenye harufu mbaya wana tatizo halisi la halitosis, kati ya asilimia 5 hadi 72 wanaofika katika huduma za afya hugundulika kuwa hawana tatizo hilo moja kwa moja.

Tatizo la kutoa pumzi yenye harudu mbaya ambalo ndiyo halitosis halisi huwa linasababishwa na uwapo wa mrundikano wa bakteria katika uvungu wa mafizi na nyuma ya ulimi jirani karibu na koo.

Kinywa kwa ujumla, ikiwamo meno, fizi, ulimi na vifuko vya mate yanaweza kuwa ni maficho mazuri kwa mamia ya bakteria.

Ndio maana inaaminika tatizo la harufu mbaya mdomoni ni kinywa chenyewe.

Kinywani pekee kuna karibu jamii 600 za bakteria ambao huambatana na mabaki ya vyakula tunavyokula kila siku.  Uwapo na protini ya kwenye mate na protini ya vyakula tunavyokula, uvunjwaji wa mabaki yake na bakteria waliopo mdomoni ni chanzo cha kuwapo kwa harufu mbaya.

Mabaki ya protini mdomoni ambayo huvunjwavunjwa na bakteria na kuwa tindikali ya amino na hapo baadaye inapovunjwa, hutoa gesi yenye harufu mbaya.

Mfano mzuri ni pale protini ijulikanayo kama methionine na cysteine inapovunjwa vunjwa kinywani huweza kutoa gesi yenye harufu mbaya ijulikanayo kama hydrogen sulphide.

Mara nyingi harufu ya kinywa inaweza kuwa nzito Zaidi baada ya kuamka ni kwa sababu wakati wa kulala mdomoni kunakuwa na kiasi kidogo cha hewa ya oksijeni.

Bakteria waliopo mdomoni ni wale wasiohitaji hewa ya oksijeni, hivyo kipindi cha usiku tuiwa tumelala ndipo huvunjavunja mabaki ya chakula ambayo huambatana na kutolewa gesi zenye harufu mbaya.

Vilevile, harufu ya kinywa inaweza kubadilika kutokana na vyakula tunavyokula vikiwamo vitunguu maji, vitunguu swaumu, iliki, tangawizi na pia uvutaji sigara na unywaji wa pombe.

Hivyo si mara zote kupumua harufu isiyo ya kawaida, bali mara nyingine inakuwa tatizo la muda tu lililochangiwa na vyakula na matumizi mengine ya vitu.

Kwa asilimia 10 zilizobaki mara nyingi husababishwa na matatizo mengine ikiwamo magonjwa ya kooni, puani, shambulizi za nyufa za mifupa iliyopo usoni, magonjwa ya mfumo wa chakula, magonjwa katika mapafu, magonjwa ya masikioni na madhara ya ugonjwa sugu wa mafindofindo (tonsillitis).

Pia, uwapo wa majipu ya fizi/meno, vidonda mdomoni au michubuko, vidonda vya kooni, huambukiza virusi vya herpes simplex na HPV.  Mara chache pia tatizo hili linaweza kuchangiwa na magonjwa ya ini ikiwamo kuharibika kwa ini na majipu katika ini.

Mara nyingine wanaolalamika tatizo hili hubainika kuwa ni tatizo la usafi wa kinywa.  Na wanaposhauriwa kuboresha usafi wa kinywa kwa kutumia dawa za meno, au kusukutua na dawa maalum za kusafisha kinywa nyuma ya ulimi, tatizo huweza kuisha haraka.

Inapotokea tatizo hilo chanzo chake sio mdomoni, ni vigumu kuweka bainisho sahihi na vilevile hata kutibika kwake inakuwa vigumu.

Uchunguzi wa tatizo hili huanzia kwa mhusika mwenye we kwa kueleza historia ya tatizo kisha wataalam wa kinywa au daktari wa kawaida humchunguza kwa kumfanyia majaribio na vipimo kadhaa.

Baada ya wataalam wa afya kujua bainisho la ugonjwa ndipo ushauri na matibabu huanza.  Kama chanzo cha harufu mbaya ni maradhi ambayo si ya kinywani, wataalam wa afya watakupa matibabu ya kutibu chanzo hicho.

Kama chanzo cha kutoa pumzi yenye harufu mabya ni kinywa, wahudumu wa afya watamuelekeza mgonjwa mambo mbalimbali kama ifuatavyo;

Kuhakikisha kupiga mswaki katika ulimi mara mbili kwa siku kwa kutumia mswaki laini, kifaa kama kijiko kwa ajili ya kukwangua uso wa ulimi, vilevile kutumia dawa yenye kiambata cha kuua bakteria.

Ulaji wa kifungua kinywa chenye afya ikiwamo kula matunda na mboga za majani yenye nyuzi nyuzi husaidia kusafisha kinywa eneo la nyuma ya ulimi wakati wa kumezwa.

Utafunaji wa bazooka unasaidia kuufanya mdomo usiwe mkavu na hewa ya oksijeni kuingia kinywani kwa wingi, vilevile utafunaji wa bazooka huweza kusaidia kutiririka kwa mate kwa wingi yanayosaidia kusafisha kinywa na kuua vimelea vya maradhi.

Mdomo ukiwa mkavu na hautafuni chochote huchangia kujiimarisha kwa bakteria wasihitaji hewa ya oksijeni.

Sukutua kwa maji mengi ikiwezekana ya uvuguvugu kila mara baada ya kula chakula, na kabla ya kwenda kulala.  Unaweza pia kutumia dawa maalum za kusukutulia kinywa zenye dawa ya kuulia vimelea.

Jaribu kuboresha usafi wa kinywa kwa kuusafisha ulimi, safisha meno kwa mswaki kila unapomaliza kula chakula, ondoa mabaki ya chakula yaliyojibana katika meno na fizi na safisha na sukutua kinywa chako kwa dawa maalum kabla ya kulala.

Unaweza kutumia vitu asilia vikiwamo majani ya miti na karafuu kama njia ya kupunguza kupumua hewa yenye harufu mbaya.

Vizuri kufanya uchunguzi wa afya ya kinywa mara kwa mara angalau kwa miezi sita mara moja ili kuweza kubaini magonjwa mbalimbali ya kinywa mapema.

No comments:

Powered by Blogger.