Umuhimu ya TOHARA kwa Wanaume
Tohara ni kitendo kinachokubalika kijamii, kidini na kwa baadhi ya tamaduni.
Kwanza ni vizuri kujua tohara ni nini?
Tohara ni upasuaji wa kitabibu ambao huiondoa ngozi ya mbele iliyochomoza kufunika kichwa cha uume. Tohara haikuanza leo, ilianza tangu zama za kale, chanzo chake ni Imani za kidini. Mpaka leo utaratibu huo umekuwa ukiendelea kurithiwa wazazi ambao huwatahiri watoto wa kiume.
Tohara inaweza kufanyika kwa mtu aliyezaliwa siku ya kwanza au ya pili. Vile vile inaweza kufanyika nyakati za watoto wakubwa mpaka utu uzima.
Upasuaji huu huchukua dakika 10 tu kwa vijana na watoto, kwa watu wazima huweza kuchukua dakika 30 mpaka saa moja. Jeraha huweza kupona kwa siku 5-7.
Kwa namna ilivyofunika huweza kuhifadhi unyevu nyevu na joto, mazingira haya ni makaribisho mazuri ya vimelea kuzaliana na kuleta madhara ya kiafya.
Mtu asiyetahiriwa, kwa ndani huzalisha vitu fulani mwilini yenye mwonekano mweupe kama maziwa yaliyokatika, uzalishaji wa taka mwili hiyo ambayo ni kisababishi cha saratani ya mlango wa uzazi kwa mwenza wa kike unayeshirikiana naye tendo la ndoa bila kutumia kinga yoyote.
Vilevile, ni kisababishi cha saratani ya uume ingawa inatokea mara chache. Hivyo aliyetahiriwa huepushwa na mambo haya mawili.
Uwapo wa ngozi hiyo huweza kutengeneza hifadhi kwa vimelea mbalimbali kuzaliana kirahisi ikiwamo bakteria, fangasi/yeast.
Wanaume wasiotahiriwa huweza kupata maambukizi ya VVU kirahisi pamoja na magonjwa ya zinaa hii ni kutokana na eneo hilo kuwa na tishu laini ambayo ni rahisi kupata michubuko.
Hupata magonjwa mbalimbali ikiwamo shambulizi la mrija wa mkojo, uambukizi kwenye njia ya mkojo (UTI), shambulizi la ngozi iliyozidi ya uume na shambulizi la sehemu ya kichwa cha uume.
Mara kwa mara mtu ambaye hajafanyiwa tohara hupata maradhi mbalimbali yanayochangia kupata muwasho kwenye uume, kuhisi muwasho kama moto na kutokwa na harufu mbaya.
Tohara inakuepusha na tatizo la kushindwa kurudisha nyuma ngozi iliyofunika uume mbele, kitabibu hujulikana kama phimosis. Faida nyingine ya tohara ni pamoja na kuyafanya mazingira ya uume kuwa masafi hivyo pia kuongeza mvuto na hamasa kwa mwenza wake.
Tohara inakufanya kuwa na muonekano mzuri na kukuongezea kujiamini.
Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa wanaume wasiofanya tohara ndio wanaopata maambukizi ya VVU kirahisi, kutahiriwa kunapunguza hatari ya kupata VVU kwa asilimia 50 – 60 kama utajamiiana na mwanamke mwenye maambukizi.
Pia, kunapunguza maambukizi ya magonjwa ya zinaa ikiwamo yale yatokanayo na virusi vya herpes na papilloma.
Madhara machache ya tohara ambayo yanaweza kujitokeza ikiwamo maumivu, kupoteza damu, kidonda kupata maambukizi, uambukizi wa mlango wa uume na kukereketa kwa uume.
Madhara haya machache hayashindi faida za kiafya za tohara, ni vizuri kwa wasiotahiriwa kujitokeza ili wafanyiwe tohara.
Baadhi ya sehemu, huduma hii inatolewa bure kama sehemu ya vita dhidi ya kuenea kwa maambukizi ya VVU.
No comments: