Header Ads

HIVI NDIO VYAKULA KUMI BORA NA FAIDA ZAKE KATIKA MWILI WA BINADAMU...!!

TUNAAMBIWA kuwa kuishi vizuri ni pamoja na kula chakula bora na sahihi. Pia, mtu anayeishi vizuri ni yule ambaye hasumbuliwi na maradhi hatari na njia pekee ya kuulinda mwili dhidi ya maradhi hatari ni kujua ipasavyo na kuvitumia vyakula bora pamoja na kufanya mazoezi.
Katika makala yafuatayo, nitakuorodhoshea baadhi ya vyakula vinavyotajwa kuwa bora (super foods) ambavyo faida zake mwilini vimeanishwa. Kwa mlaji, linakuwa jambo la busara kujua faida ya kila chakula unachoingiza tumboni. Kwa mujibu wa mwandishi wa makala kuhusu vyakula hivi bora, Bw.Hakeem Rahman, hivi ni vyakula vinavyowafanya “wenye afya nzuri kuendelea kuwa na afya nzuri zaidi na wenye afya mbovu, kuwa na afya nzuri.”



SAMAKI
Wana virutubisho aina ya Omega 3 ambavyo huulinda moyo dhidi ya maradhi. Samaki pia wana virutubisho vinavyomuongezea mlaji uwezo wa kukumbuka (memory), kuna virutubisho vyenye uwezo wa kupambana na kansa mwilini, kuongeza kinga mwilini na kuondoa mafuta mabaya mwilini (Bad cholesterol). (unashauriwa kula samaki kwa wingi kadiri uwezavyo).
Baadhi ya virutubisho muhimu vinavyopatikana kwenye samaki ni pamoja na vitamini D, vitamin 12, vitamini B3, vitamini B6, Omega 3 Fatty acids, protini na madini mengine mengi.

KARANGA
Unaweza ukazidharau karanga, lakini zina faida kubwa mwilini. Miongoni mwa faida zake ni pamoja na kuimarisha afya ya moyo, hupunguza kolestro mbaya mwilini na kuongeza kolestro nzuri. Mafuta mazuri yaliyomo kwenye karanga hupunguza shinikizo la juu la damu na huponya magonjwa ya moyo na hupunguza uzito. Faida zote hizi unaweza kuzipata kutoka kwenye karanga au siagi iliyotengenezwa kutokana na karanga (peanut butter). (unashauriwa kula kiasi kadhaa kila siku, hasa za kuchemsha ndiyo nzuri).

KAROTI
Miongoni mwa faida nyingi za karoti ni pamoja na kushusha kolestro mbaya mwilini, kupunguza unene, kuimarisha nuru ya macho, kuimarisha shinikizo la damu, inatoa kinga kwenye figo na inaimarisha sukari mwilini. (kula kadiri unavyoweza, mbichi au zilizochemshwa).

MAHARAGE YA SOYA
Haya ni maharage bora kabisa ambayo yana faida nyingi mwilini, ikiwemo kushusha shinikizo la damu, kuimarisha sukari mwilini, kupambana na ugonjwa wa kisukari, figo, moyo, kutoa kinga dhidi ya ugonjwa wa kansa ya kibofu na magonjwa mengine ya wanawake.

PAPAI, TIKITI MAJI
Miongoni mwa matunda muhimu mwilini ambayo hata mgonjwa wa kisukari anashauriwa kuyala ni pamoja na papai na tikitimaji ambayo yanaelezwa kuwa na kiwango kikubwa cha ufumwele (fibre) na hivyo kutoa mchango mkubwa sana katika kuimarisha kiwango cha sukari mwilini. (kula kiasi cha moja katika ya matunda hayo mawili, kila siku).

KITUNGUU SAUMU
Hiki ni kiungo cha mboga, licha ya kuonekana kama ni kiungo cha kuongezea ladha tu ya chakula, lakini ni miongoni mwa vyakula vyenye faida kubwa katika afya zetu. Kitunguu saumu husaidia kuyeyusha damu mwilini hivyo kumuepusha mlaji kushikwa na ugonjwa wa moyo pamoja na presha. Kitunguu hicho pia hutoa kinga kwenye ini na huondoa maumivu ya viungo. Kula angalau kitunguu kimoja mara moja kwa wiki.

ABDALASINI
Hiki nacho ni kiungo cha kuongezea ladha na rangi kwenye chakula, lakini nacho kina faida zaidi ya hiyo. Abdalasini, ambayo inapatikana kwa wingi katika masoko mbalimbali nchini, hufaa sana kutumiwa na wagonjwa wa kisukari, kwani hurekebisha kiwango cha sukari mwilini kwa kiwango cha hadi pointi 50. inapendekezwa kutumiwa angalau nusu kijiko cha chai kila siku mara mbili.

TANGO
Watu wengi hulipuuza tango na wengine hawajawahi kula kabisa kwa sababu siyo tamu sana mdomoni, hata linapochanganywa kwenye kachumbari huepukwa. Hii yote inatokana na kutokujua umuhimu wa mboga hii. Inaelezwa kuwa tango linapoliwa husaidia sana kusaga chakula tumboni hivyo kumuwezesha mlaji kupata choo laini. Halikadhalika, tango linaweza kutumika katika kuboresha ngozi ya uso kwa kupaka, kwani huondoa vipele na kuifanya ngozi kuwa nyororo. Ni zuri linapoliwa na maganda yake na unaweza kula kiasi utakachoweza.

ASALI

Kama kuna chakula kitamu na kizuri duniani, basi ni asali. Hiki ni chakula cha asili ambacho kimekuwepo enzi na enzi na kimesifiwa hata katika vitabu vya Mungu. Asali ina uwezo wa kudhibiti sumu mwilini, ina uwezo wa kumfanya mtu mnene kupungua uzito na mtu mwembamba kuongezeka uzito hadi kufikia uzito wa kawaida. Asali huupa nguvu mwili haraka, huifanya ngozi kuwa nyororo, huzuia asidi, husafisha damu na ina uwezo wa kuua vijidudu mwilini. Lamba asali kijiko kimoja cha chai asubuhi kabla hujala kitu chochote. Kwa kuwa asali ni tamu lamba mara 3, wagonjwa wa kisukari wanashauriwa kuila kwa tahadhari.

TENDE

Tende, ambayo ni maarufu sana katika nchi za arabuni na ukanda wa mwambao wa Tanzania, ni miongoni mwa vyakula vyenye faida kubwa mwilini. Sifa ya kwanza ya tende ni uwezo wake wa kuupa nguvu moyo dhaifu na kuupa nguvu mwili (energizer). Wale wenye matatizo ya moyo kukosa nguvu tende zitawasaidia. Tende nayo ni mlo tosha unaopaswa kuwepo katika orodha ya milo yetu ya kila siku.
Katika maisha tunayoishi hivi sasa, ili mtu kuupa mwili wako kinga imara dhidi ya maradhi mbalimbali na ya hatari, hatuna budi kuzingatia ulaji wa vyakula mchanganyiko vya asili na kuacha kupenda kula vyakula visivyokuwa na faida katika miili yetu ambavyo mara nyingi tunapenda kuvila, kwa sababu ni vitamu mdomoni.

No comments:

Powered by Blogger.