Header Ads

Kulika Kwa Meno- sehemu ya 1

Matokeo ya picha ya ugonjwa wa meno
Kulika kwa meno ni hali ambapo sehemu ngumu ya nje ya meno huondoka na kusababisha sehemu ya ndani kuwa wazi. Tatizo hili huanza kwa kuondoka sehemu ngumu ya nje (enamel) na kuiweka wazi sehemu ya kati ambayo ni ngumu pia (dentine). Tatizo likiendelea bila matibabu hufanya kiini cha jino, sehemu ambayo kuna mishipa ya damu, mishipa ya fahamu na chembe chembe mbali, kuwa wazi (dental pulp exposure).

Dalili hutegemea na kiwango cha ulikaji wa jino. Ikiwa ni sehemu ya nje kabisa imetoka, dalili huweza kuwa msisimko (sensitivity) wakati wa kunywa vinywaji vya baridi, vya sukari na hata meno yakipulizwa na upepo. Kama kiini cha jino kitakuwa wazi basi maumivu huanza na yanaweza kuwa makali kabisa.

Matibabu hutegemea kiwango cha uharibifu. Kama uharibifu ni kidogo, utumiaji wa dawa za meno zenye madini zaidi hasa ya fluoride unaweza kuondoa dalili. Wakati mwingine kutumia dawa za kupaka kitaalam, kuziba na kuvalisha kofia ngumu (crown) meno husika na mwisho ni kufanya matibabu ya mzizi wa jino (root canal treatment) au kung’oa jino kama kiini cha jino kimebaki wazi.

Ziko aina mbali mbali za kulika kwa meno kutokana na nini kinasababisha tatizo, na kinga au tiba hutegemea nini kisababishi.

Kusagika kwa meno (attrition)

Huku ni kulika kwa meno kwenye sehemu ambapo meno ya juu na chini hukutana (occlusal surfaces). Katika hali ya kawaida meno hulika sehemu hizi kutokana na kadri yanavyoendelea kutumika kusaga vyakula. Hali hii huendelea polepole kadri mtu anavyoendelea kuishi (umri), kitaalamu inajulikana kama physiological attrition.
Si rahisi kuhisi dalili zake kwani mwili hujaribu kuziba vitundu vya mifereji midogo inayotoka kwenye kiini cha jino kwenda kwenye sehemu ngumu ya kati (dentine). Ni vitundu hivi ambavyo vikiwa wazi husababisha msisimko (sensitivity). Kulika kwa meno sehemu ya kusaga huwa ugonjwa pale tu unapotokana na mambo mengine zaidi ya kule kwa kawaida kwa kuongeza umri.

Sababu za kusagika kwa meno (attrition)

Baadhi ya mambo yanayosabisha hali hii ni
Kusaga meno (bruxism): - hii ni hali ambayo mtu husaga meno yake wakati hatafuni kitu chochote na mara nyingi mtu huwa hajitambui kama ana tatizo hili. Hali hii mara nyingi hujitokeza wakati wa usiku mtu akiwa amelala (nocturnal bruxism) japo kwa wachache wanaweza saga mchana pia. Si rahisi mtu wa namna hii kujitambua mpaka pale atakapoambiwa na mtu wanayelala pamoja au atakapo kwenda kwa mtaalamu wa meno na kuelezwa.

Nini husababisha hali hii?

Yapo baadhi ya mambo yanayoweza kusababisha tatizo hili ingawa zaidi linahusishwa na mabadiliko ya kisaikolojia. Watu wenye mawazo mengi wanaonekana kuwa kwenye hatari zaidi ya kupatwa na tatizo hili.

Tatizo hili pia linaweza kutokana na jino lililozibwa na kujazwa zaidi ya kawaida. Mwili hufanya harakati za kupungua sehemu iliyozidi kwa kuisaga na hatimaye kujikuta umejenga mazoea, kiasi kwamba hata jino likisha kuwa kiasi sawa bado mwili utaendelea kusaga tu.

Pia wale wanaokaa kwenye meza kwa muda mrefu wakisoma au vyovyote huku wameshikiria kidevu kwa nguvu, nao ni waathirika wa ugonjwa huu. Katika hali ya kawaida mtu ukiwa umefunga mdomo umetulia meno ya juu na ya chini huwa hayakutani bali huacha nafasi kama milimita mbili hivi (resting space). Sasa ukiyabana pamoja kwa muda mrefu kwa kushikilia kidevu, utayafanya yajenge mazoea ya kushikana hata pale ambapo hujashika kidevu na mwishowe kuanza kusagana.

Dalili zake na viashiria vyake

Mgonjwa mwenyewe kuhisi msisimko wakati wa kunywa vitu vya baridi, maumivu kama kiwango cha uharibifu ni kikubwa kiasi cha kuacha kiini jino wazi (dental pulp exposure). Ukiangalia meno utakuta yamelika sehemu ya kutafunia kwenye magego na visaidizi vyake (molars and premolars), sehemu za kukatia na kuchoma kwa meno ya mbele (canines and incisors).
Kusagika huanzia sehemu za meno zilizoinuka (cusps) ambazo hatimaye huondoka kabisa na kuwa bapa au flati. Meno huweza kusagika mpaka wakati mwingine kufikia kwenye usawa wa fizi. Watu wenye tatizo hili huonekana kuwa na uso wa mraba kutokana na msuli mkubwa wa kuvuta taya (masseter muscle) kunenepa kutokana na kutumika zaidi. Mgonjwa pia huweza kuchoka kirahisi misuli wakati wa kutafuna katika hali ya kawaida.
Tatizo linaweza kuathiri hata sehemu ya muunganiko wa taya la chini na fuvu (temporomandibular joint - TMJ).
Mgonjwa huweza kusikia maumivu kwenye kiungo (joint) hiki na wakati mwingine kufyatuka fyatuka (TMJ dislocation) au kutoa sauti wakati wa kufungua na kufunga kinywa (popping or cricking sound in TMJ).
Picha zikionyesha meno yaliyosagika
picha ya juu-kinachoonekana kama kuvimba shavu ni msuli wa kuvuta taya (masseter muscle) ulioongezeka ukubwa kutokana na kusaga meno. Picha ya chini mwezi mmoja baada ya kupata matibabu ya uhakika, msuli unarudi katika hali ya kawaida.

Matibabu

Ni vizuri kujua chanzo cha tatizo hili na kukishughulikia kwanza kabla ya kufanya matibabu zaidi ya meno kurekebisha uharibifu uliotaka na msagiko. Utafiti unaonesha  wengi wenye matatizo haya ni wenye mawazo yaliyozidi kiwango (stress). Lazima ujue kwanini mtu anawaza sana ili ummpatie ushauri nasaha au hata kumpeleka kwa wataamu wa mambo ya saikolojia ili waweze kumsaidia.
Wakati hayo yakiendelea inabidi kumfundisha mgonjwa kulegeza taya (relaxation exercise) na kuachanisha meno kila anapohisi meno ya juu na ya chini yamekutana. Akifanya mazoezi haya kwa muda mrefu mwili huweza kujenga mazoea kuwa kila meno yakikutana yaachanishwe (conditioned reflex action).
Mgonjwa akiacha kusaga basi matibabu ya kurekebisha madhara yanaweza kufanyika kwa mafanikio makubwa, iwe kuziba, kuua mzizi wa jino na kuyavalisha meno kofia ngumu hasa metal reinforced porcelain crown.

Kwa wale ambao ni vigumu kuacha tabia ya kusaga wanaweza kutengenezewa kifaa maalumu cha kulinda meno wakati wa usiku (night guards), ambacho huvaliwa na mgonjwa usiku wakati wa kulala kuzuia meno kugusana na baada ya muda atazoea pia na kuacha kusaga. Kifaa hiki husaidia pia kuondoa matatizo yaliyokwisha jitokeza kwenye jointi.
      
                                                                                                      kifaa cha kukinga meno  yasisagane         mgonjwa akiwa amevaa kifaa
Ni vizuri kumuuliza mwenzako kama amewahi kukusikia ukisaga meno usiku ili uweze kuchukua hatua za kuwaona wataamu mapema. Kumbuka kujua tatizo mapema na kulitibu ni sehemu ya hatua za kinga.

Niishie hapa kwa leo, siku nyingine nitaongelea aina nyingine za kulika kwa kwa meno kama kuyeyuka kwa meno (tooth erosion), abrasion na abfraction wakati huo nitakuwa nimejaribu kupata maelezo ya “abfraction  na abrasion” kwa Kiswahili.0765203999

No comments:

Powered by Blogger.