Fahamu juu ya tatizo la kutopata ujauzito
Ni tatizo kubwa katika jamii kwani kila mmoja anataka afikie malengo ya kuwa na familia.
Mwanamke na mwanamume wote wanahusika katika tatizo hili japo mara nyingi huonekana ni la mwanamke. Kutoshika mimba kwa muda mrefu ni ugumba ua infertility kwa kitaalamu. Mwanamke au mwanaume anaweza kuwa mgumba.
Ugumba umegawanyika katika maeneo makuu mawili. Kwanza ni ‘primary infertility’ ambapo mwanamke hana historia ya kuwa na mimba wala mwanaume hana historia ya kumpa mwanamke mimba.
Ugumba wa aina ya pili ni ‘secondary infertility’ ambapo mwanamke anayo historia ya kuwahi kupata ujauzito, haijalishi kama alizaaa au mimba ilitoka na mwanamume anayo historia ya kumpa mwanamke mimba na pia haijalishi kama mtoto alizaliwa au mimba ilitoka.
Tatizo la mwanamume kutoweza kumpa mwanamke mimba linaweza kusababishwa na kukosa nguvu za kiume hivyo kushindwa kufanya tendo la ndoa.
Hali hii ya kukosa nguvu inaweza kusababishwa na matatizo mbalimbali kwani yenyewe si ugonjwa.
Kwa hiyo kitu cha msingi siyo kuongeza nguvu bali ni kufanya uchunguzi kuona tatizo ni nini na kulipatia ufumbuzi.
Tatizo lingine kwa mwanamume ni kutotoa mbegu za kiume za kutosha ua kutoa mbegu zisizo na ubora.
Hii ni baada ya kupima kipimo cha mbegu za kiume. Mbegu zinaweza zisizalishwe ua zikazalishwa pasipo na ubora unaostahili kurutubisha yai la mwanamke.
Matatizo mbalimbali yanaweza kuathiri uzalishaji wa mbegu za kiume kama uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe kali, maumivu ya korodani na utumiaji wa dawa za kulevya kama mirungi na bangi.
Mazingira ya joto katika korodani pia huathiri uzalishaji wa mbegu. Kutofahamu mzunguko wa hedhi wa mwanamke na kipindi gani mwanaume anaweza kumpa mimba ni changamoto nyingine kwa upande wa mwanaume.
Kwa upande wa mwanamke zipo sababu nyingi zinazoweza kusababisha awe na tatizo la kutopata ujauzito.
Miongoni mwa sababu hizo ni pamoja na matatizo katika mfumo wa homoni. Mwili wa mwanamke hutawaliwa na hizi homoni ambazo ni kemikali za asili ndani ya mwili.
Mabadiliko madogo yakitokea wakati wa kuzalishwa kwake au kuzalishwa wakati ambao si muafaka huweza kusababisha ashindwe kupata ujauzito.
Lipo pia tatizo la mwanamke kuwa na uzito mdogo au mkubwa kupita kiasi kutokana na mfumo wa ulaji na mazoezi ya mwili. Mambo haya huathiri uzalishaji wa kawaida wa homoni.
Ikumbukwe pia kuwa uwezo wa kupata ujauzito hupungua kadri umri unavyozidi kuongezeka tangu kipindi anapovunja ungo.
Hii hutokana na hupungua kwa uzalishaji wa homoni husika. Kuanzia miaka 35 na kuendelea huwa kunakuwa na tatizo la kupata ujauzito kwa wanawake wengi hasa wale ambao hawajawahi kabisa kupata mimba.
Umri wa ukomo wa kupata hedhi kwa asilimia 80 ya wanawake ni miaka 45. Wapo wachache kati ya asilimia 20, ambao ukomo wao wa kupata hedhi huwa juu au chini ya miaka 45 na kwa nadra sana wapo wanawake kwenye asilimia hizo ambao aghalabu huweza kupata ujauzito.
Kuziba kwa mirija ni hali nyingine ambayo huweza kumzuia mwanamke kupata ujauzito. Hali hii huwa mbaya zaidi kama mirija yote miwili imeziba baada ya kuthibitishwa na kipimo maalumu.
Kuziba kwa mirija husababishwa na maradhi yaambikizwayo katika nyonga ya mwanamke. Mengi ya maradhi haya ni yale yatokanayo na kujamiiana ambayo hayakugundulika mapema ili yapate tiba kama vile kisonono.Mirija pia inaweza kuziba baada ya kufanyiwa upasuaji wa tumbo unaohusu au usiohusu sehemu ya nyonga.
Mara nyingi wanawake ambao mirija yao imeziba huwa hawanyeshi dalili zozote za kuziba huko. Ni mpaka kipimo maalumu cha mirija kifanyike ili kujua uwepo wa hali hiyo.
Katika hali ya kawaida, ute unaopatikana kwenye kizazi cha mwanamke huwa na sifa ya kuruhusu mbegu za kiume ziweze kusafiri kwa urahisi na kulifikia yai ili kulirutubisha.
Hali hii hufanyika ndani ya mirija ya uzazi. Kwa baadhi ya wanawake ute huu huwa na uzito na kemikali ambazo ni vigumu kwa mbegu za kiume kupita kwa urahisi.
Wakati mwingine mwili wa mwanamke huzalisha sumu ambazo huziua mbegu za kiume. Haya yote husababisha kukutana kwa yai na mbegu za kiume kusitokee na hivyo mwanamke kutokupata ujauzito.
Zipo pia sababu za kimaumbile na uwepo wa uvimbe kwenye mfuko wa uzazi na via vya uzazi kwa ujumla.
Hali hii hujitokeza saidi kwa wanawake wenye umri mkubwa wa kuanzia miaka 30 na kuendelea. Uwezo wa kupata, kutunza au kupata na kutoka kwa ujauzito hutegemea aina ya uvimbe, sehemu ulipo, idadi na ukubwa wa uvimbe.
Hivyo, si wanawake wote wenye uvimbe au vimbe ambao hushindwa kupata ujauzito. Vilevile sio wote wanaopata ujauzito wakiwa na uvimbe. Mara nyingi akiwa na uvimbe ujauzito huishia kutoka.
Matibabu ya saratani pia huweza kuathiri uwezo wa mwanamke kupata ujauzito. Hali hii hutegemea aina ya tiba inayohusika kama ni matumizi ya dawa, mionzi, upasuaji au mchanganyiko wa njia mbili au zote kati ya hizo.
Asilimia kubwa ya matatizo ya mwanamke kutokuwa na uwezo wa kupata ujauzito huweza kutibika iwapo njia sahihi za utatuzi zitafuatwa.
Mengi ya matatizo haya huhitaji uchunguzi na ufuatiliaji wa kina. Ni vizuri kuonana na wataalamu wa afya ana kwa ana mapema ili kujua chanzo cha tatizo na kupatiwa msaada unaostahili.
0765203999
No comments: