Header Ads

HOMA YA DENGU

Dengu ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vinavyoenezwa na mbu jike wa jamii ya Aedes aegypti na kwa kiasi kidogo mbu wa Ae albopictus. Mbu hawa pia huambukiza virusi vya homa ya manjano (yellow fever) na zika. Mbu hawa hupatikana zaidi katika maeneo ya joto hususani maeneo ya mijini.




Maambukizi ya ugonjwa
Virusi vya ugonjwa wa dengu huambukizwa kwa mbu, mbu jike wa jamii ya Aedes aegypti akimng’ata mgonjwa, hubeba vijidudu vya dengu, vijududu hivi hukaa kwa mbu kwa siku 4-10 na baada ya hapo mbu huyu huweza kuambukiza huu ugonjwa kwa kila anayemng’ata kwa kipindi chote cha maisha yake.

Watu walioambukizwa virusi hivi (walio na dalili na wale wasio na dalili) ndio hubeba virusi vya ugonjwa wa dengu ambavyo huchukuliwa na mbu pale wanapong’atwa. Wagonjwa wa dengu wanaweza kuendelea kuambukiza wengine kupitia mbu kwa muda wa siku 4-5, na si zaidi ya siku 12 tangu walipopata dalili za ugonjwa wa dengu.

Makazi ya mbu wanaosambaza ugonjwa wa dengu
Mbu wanaosambaza ugonjwa wa dengu huishi na kuzaliana kwenye maji yaliyotuama kenye vyombo vinavyotelekezwa na binadamu, mfano vifuu, chupa, ndoo n.k Mbu hawa hung’ata wakati wa mchana, hasa wakati wa asubuhi na jioni kabla ya giza. Mbu jike huweza kung’ata watu wengi katika zoezi la kutafuta chakula. Mayai ya mbu huyu huweza kukaa kwa zaidi ya mwaka mmoja yakiwa yamekauka na hutoa vilui lui yanapopata maji.

Dalili za ugonjwa wa dengu
Dengu hushambulia watu wote kuanzia watoto mpaka wazee. Husababisha homa kali (nyuzi joto 40oC) inayoambatana na maumivu makali ya kichwa, maumivu nyuma ya macho, maumivu ya misuli na viungo, kichefu chefu, kutapika, kuvimba tezi na vipele. Dalili hizi hudumu kwa muda wa siku 2-7, na hutokea siku 4-10 baada ya kung’atwa na mbu.

Asilimia moja ya wagonjwa hupata dengu kali (severe dengue) za ugonjwa huu ambazo huweza kusababisha kifo, na hizi hutokana na kupata athari katika mifumo mbali mbali ya mwili. Dalili za ugonjwa wa dengu kali ni pamoja na kutapika mfululizo, kupumua haraka haraka, kutoka damu kwenye fizi, uchovu na kutapika damu. Wagonjwa wenye dalili hizi wanahitaji matibabu ya hali ya juu ya kusaidia mifumo ya mwili inayoshindwa kufanya kazi na wako mahututi.

Matibabu ya dengu
Hakuna matibabu maalumu ya dengu, matibabu yake ni ya kutibu dalili zinazosababishwa na huu ugonjwa. Kwa kiasi kikubwa wagonjwa huptatiwa matibabu yafuatayo

Dawa za maumivu: dawa nzuri ni paracetamol, haishauriwi kutumia dawa za kundi la diclofenac, ibuprofen, muvera, meloxicam au indomethacin kwani hizi huathiri utendaji wa chembe zinazozuia damu kutoka mwilini
Kunywa maji kwa wingi, na wakati mwingine kuwekewa maji mwilini hasa pale unapotapika sana
Wagonjwa wachache wanaopata dengu kali huhitaji uangalizi wa karibu na matibabu katika hospitali. Wagonjwa hawa wanakuwa na hatari ya kupoteza uhai wao.

Kinga baada ya kuugua dengu
Kuna aina nne tofauti za virusi vinavyosbababisha dengu (DEN-1, DEN-2, DEN-3 na DEN-4) mgonjwa aliyeambukizwa aina moja ya virusi vya dengu hupata kinga ya kudumu dhidi ya aina hiyo ya virusi alivyoambukizwa. Mgonjwa huyu anaweza kuugua tena iwapo ataambukizwa na aina nyingine za virusi.

Kujikinga na dengu
Njia bora ya kujikinga na ugonjwa huu ni kuzuia kung’atwa na mbu wanaoueneza, hili linaweza kufanikiwa kwa

Kuzingatia usafi wa mazingira ikiwa ni pamoja na kufyeka majani marefu yanayozunguka maeneo ya makazi ya binadamu
Kuzuia mazalio ya mbu; kuondoa vyombo au vifaa chakavu vinavyotuamisha maji katika mazingira ya nyumbani na makazi. Vitu hivi ni pamoja na chupa, vifuu, makopo n.k
Mazalio ya mbu ni hatari kwa kuwa huweza kuhifadhi mayai ya mbu kwa kipindi kirefu kinachofikia mwaka mmoja, hivyo uondoaji wa hivi vifaa si wakati wa masika au mvua pekee.
Kuhakikisha milango na madirisha hayaruhusu mbu kuingia ndani; matumizi ya nyavu za kuzuia wadudu kwenye milango na madirisha. Pia kupuliza dawa ndani ya nyumba ili kuwaua mbu wanaong’ata mchana
Kutumia vyandarua vilivyowekwa dawa pale unapolala mchana, hii ni muhimu kwa watoto wadogo
Kujikinga na mbu wakati wa mchana hasa asubuhi na jioni; kuvaa nguo zinazofunika mwili, kutumia dawa za kupaka au kuweka kwenye nguo za kufukuza mbu (mosquito repellants)
Ushauri kwa wagonjwa wenye dalili za dengu
Ugonjwa wa dengu hauna tiba maalumu, tiba yake ni ya kutibu dalili zinazotokea baada ya kuugua. Hospitali nyingi hazina vipimo vya kutambua huu ugonjwa, hivyo madaktari na wahudumu wa afya wanapomhudumia mgonjwa mwnye dalili za dengu hufanya vipimo vya kuangalia kama wana magonjwa mengine yanayofanana na dengu mfano malaria, maambukizi ya njia ya mkojo (UTI) na homa ya tumbo (typhoid fever). Pale wanapopata majibu ya vipimo vya magonjwa haya na kugundua hayakuonekana humpatia mgonjwa matibabu ya kutibu dalili alizonazo nazo na mara nyingi hizi ni zilie za dengu. Mgonjwa mwenye dalili za dengu akizingatia haya matibabu hali yake itakuwa nzuri baada ya muda mfupi, hakuna sababu ya kuzunguka hoapitali nyingi kutafuta kipimo cha dengu kwa kuwa matibabu yatakayotolewa ni haya ya kutibu dalili hata baada ya kipimo kuonyesha una maambukizi ya dengu.

Mgonjwa anayepata matibabu ya dengu akiona dalili zinaongezeka na hali yake inakuwa mbaya anatakiwa aende hospitali, hali kama hii inaweza kutokea pale mgonjwa anapopata dengu kali.

No comments:

Powered by Blogger.