HIZI NI SABABU ZINAZOPELEKEA MTU KUPATA SHAMBULIZI LA MOYO! ZIFAHAMU KUEPUKANA NA TATIZO.
Shambulizi la moyo ni tatizo linalotokea kwenye moyo na ni matokeo ya sehemu ya misuli ya moyo kukosa damu ya kutosha. Kushindwa kufikiwa kwa damu katika misuli hii kunapelekea shughuli nyingi zinazofanywa na misuli hii
kusimama jambo ambalo hupelekea matatizo mengi ya kiafya na hata kifo.
Sayansi ya moyo wa binadamu na mzunguko wa damu.
Ukuta wa Moyo wa binadamu umeundwa kwa tishu za misuli yenye uwezo wa kusinyaa na kutanuka, una mishipa ya damu ambayo husambaza damu katika moyo wenyewe(mishipa hii huunda mfumo wa mzunguko wa damu wa ndani ya moyo-'coronary circulation'), ina vyumba vya wazi vinne 2 upande wa kushoto na 2 upande wa kulia, moyo umeunganishwa na misipa mbalimbali ya damu ambayo hutoa na kuingiza damu katika moyo mishipa hii ni pamoja na aorta, vena cava, mishipa inayotoka na kuingia ambayo imeunganishwa na mapafu.
Aorta ndio mshipa mkubwa unaotoa damu safi kutoka katika moyo kuelekea sehemu nyingine za mwili, moja ya matawi ya mshipa huu husambaza damu katika moyo. tawi hili huitwa (coronary vessel).
Damu inayopita katika mshipa wa aorta imebeba hewa safi ya oksijeni ambayo ina kazi nyingi na muhimu katika seli, moja ya kazi za oksijeni katika seli ni kuunguza chakula ili kujipatia nishati ambayo inazifanya seli hizi ziendelee kufanya shughuli mbalimbali za mwili. Bila hewa hii ya oksijeni hakuna seli itakayoweza kupata nishati ya kutosha kuendelea kufanya kazi.
Shambulizi la moyo linatokeaje?
Kama ilivyoainishwa hapo awali kuwa shambulio la moyo ni pale sehemu fulani ya moyo inakosa kufikiwa na damu, damu ambayo imebeba kemikali muhimu ya oksijeni. kushindwa kufikiwa na damu katika sehemu hizo kunafanya seli za maeneo yaliyoshindwa kufikiwa na damu kufa na kutengeneza kovu. Sehemu ya moyo ambayo imetengeneza kovu inapoteza uwezo wa kufanya kazi ingawa sehemu nyingine ambazo hazijaathiriwa zitaendelea na utendaji kazi kama kawida. Kwa kuwa tayari kiwango cha seli zinazoshughulika katika moyo zimepungua hivyo basi hata utendaji kazi wa moyo utadhoofu.
Ikiwa sehemu zitakazoathiriwa ni zile pande za chini za moyo, pande ambazo ndio hufanya kazi kubwa ya kusukuma damu jambo hili hupelekea moyo kusimama na hatimaye kifo.
Kumbuka kufa kwa seli za sehemu fulani ya moyo kunaweza kuambukiza sehemu jirani na hatimaye tatito kuwa kubwa kiasi cha kuhatarisha muhai.
Nini husababisha shambulizi la moyo?
- Tatizo la moyo kufikiwa na kiwango kidogo cha damu ambacho hakibebi oksijeni inyokidhi mahitaji ya seli za moyo. Tatizo hili kitaalamu linaitwa ANGINA. ni tatizo ambalo mtu anakuwa nalo na tatizo hili likiwa sugu linaweza kupelekea seli za moyo kufa na hatimaye shambulizi la moyo kutokea.
- Kuwa na kiwango kikubwa cha rehemu mwilini. Rehemu inapozidi mwilini huweza kusababisha madhara mengi ya kiafya huku kubwa ikiwa ni kutengeneza pande la mafuta ambalo linaweza kuziba mishipa ya damu a kuzuia damu kufika upande wa pili wa mshipawa damu. Mishipa inyosambaza damu katika moyo hushambuliwa zaidi na rehemu kwa sababu ni mishipa miembamba mno.
- Matatizo ya kisukari- watu wenye matatizo ya kisukari hushambuliwa zaidi na shambulizi la moyo kwa kuwa watu hawa huwa na kiwango kikubwa cha sukari ambayo huongeza shinikizo la damu ambalo huweza sababisha mishipa ya damu kupasuka.
- Matumizi ya vyakula ambavyo vina kiwango kikubwa cha mafuta ya wanyama mafuta ambayo ndio yenye kiwango kikubwa cha rehemu.
- Matatizo ya shinikizo la damu- watu wenye msukumo wa damu usio wa kawaida(mkubwa) wako katika hatari zaidi ya kupata shambulizi la moyo kwa kuwa shinikizo la damu huaribu mishipa mbalimbali ya damu ikiwemo ya moyo.
- Watu wenye uzio mkubwa na fetma(kitambi)- watu hawa huwa katika hatari zaidi kwa sababu kitambi ni chakula cha ziada ambacho mwili umeshindwa kukitumia kwa vile hakikuhitajika na hivyo basi mwili hukihifadhi chakula katika mfumo wa mafuta katika sehemu mbalimbali ikiwemo katika moyo. Mafuta haya huweza kuziba mishipa ya damu mwilini.
- Uzembe na uvivu- watu ambao hawafanyi mazoezi au kujihusisha na shughuli mbalimbali za kimwili wako katika hatari pia kwa kuwa kwa kutokufanya hivyo wanakaribisha mlundikano wa mafuta mwilini.
- Mitindo mbalimbali ya maisha kama ulevi, uvutaji, msongo wa mawazo huweza sababisha shambulizi la moyo.
- Watu wenye matatizo ya upungufu wa kinga mwilini kama UKIMWI, watu walio na historia ya kuugua magojwa ya moyo pamoja na watu wenye umri mkubwa wa kuanzia miaka 55 hawa wako katika hatari zaidi.
No comments: