Header Ads

JINSI VYAKULA TULAVYO VINAVYOTUMALIZA

KATIKA makala zetu zilizopita, tulishaelezea madhara ya kula ugali uliotokana na mahindi yaliyokobolewa, tuliona kwamba chakula hicho kinapoingia mwilini hugeuka na kuwa sukari ambayo baadaye huweza kusababisha ugonjwa wa kisukari. Mgonjwa wa kisukari hukatazwa kula ugali wa aina hii na badala yake hutakiwa kula ugali wa dona, mtama au ulezi.



Kwa faida ya afya zetu na kwa ajili ya kuimarisha kinga ya miili yetu, sote tunatakiwa kula ugali wa dona, mtama au ulezi kabla hata ya kuugua. Vyakula hivi ni muhimu sana na siyo vya kimasikini kama ambavyo watu wengi wanadhani. Kwa bahati mbaya, upatikanaji wa unga wa dona umekuwa mgumu na ghali kuliko sembe nyeupe, hivyo kuwafanya watu wengi kukimbilia sembe nyeupe ambayo inapatikana kirahisi kila kona ya nchi na kwa bei nafuu.

Kwangu mimi naliona tatizo hili ni la kitaifa na kisera. Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ilipaswa kutoa elimu ya kutosha ya kuelezea madhara yatokanayo na ulaji wa sembe nyeupe kisha kuweka sera itakayokataza uzalishaji wa kibiashara wa sembe nyeupe kama ilivyo sasa. Sera ya namna hii ingeokoa maisha na afya za Watanzania wengi wanaoteketea kila situ kutokana na ugonjwa wa kisukari.

Naamini kaya nyingi nchini hazijui kabisa kama ugali utokanao na sembe nyeupe wanaokula kila siku iendayo kwa Mungu, una madhara kiafya. Ni vigumu kuzieleza na zikakuelewa familia ambazo kwa maisha yao yote zimekuwa zikiamini kwamba kula ugali mweupe ndiyo kitu bora.

Serikali ilipaswa kuliangalia suala hili na kuona kama janga la kitaifa, ilipaswa kuanzisha kampeni maalum ya kutoa elimu kuhusu vyakula na lishe kwa njia mbalimbali, zikiwemo za matangazo redioni na kwenye televisheni.

ULAJI WA MATUNDA NA MBOGA
Hakuna kitu muhimu kwa mwili wa binadamu kama kujenga kinga ya mwili. Mwili unapokuwa na kinga imara, si rahisi kuugua magonjwa ya ajaba. Miongoni mwa kazi nyingi za matunda na mboga za majani, ni pamoja na hiyo kazi ya kujenga mwili na kuujengea uwezo wa kujikinga wenyewe.

Pamoja na umuhimu huo, ni watu wachache sana hula matunda na kuyachukulia kama sehemu ya milo yao ya kila siku. Watu wengi hula matunda au mboga za majani ‘kwa bahati mbaya’, huona siyo chakula muhimu sana. Hili ni kosa kubwa miongoni mwa makosa mengi yanayofanywa na watu katika masuala ya afya.

Matunda yanatakiwa kuliwa kila siku na kwa wingi, vivyohivyo mboga za majani. Unapoacha kula matunda na mboga za majani za aina mbalimbali, jua unaukosesha mwili wako kinga dhidi ya maradhi yanayoweza kujitokeza mwilini.

VYAKULA HIVI NDIYO VINAVYOTUMALIZA

Vyakula tunavyotakiwa kuvila, hatuvili tena na pengine upatikanaji wake ni wa shida, hivyo tunalazimika kula vilivyopo licha ya kuwa vina madhara kwa afya zetu. Hali hii imeongeza idadi ya wagonjwa na magonjwa sugu.

Chakula kikuu cha mijini ni chips, kuku, mayai, soda, juisi za makopo au paketi, nyama choma na pombe. Pia kuna mkate mweupe, maandazi na chapati. Vyakula hivi huliwa kila siku, lakini ukivichambua utagundua havina faida yoyote mwilini zaidi ya kuingia na kutengeneza maradhi.

No comments:

Powered by Blogger.