Header Ads

RATIBA BORA YA MILO KWA MTOTO NA MAMA MJAMZITO

Mlo kamili (balanced diet), ni muhimu kwa ajili ya maendeleo mazuri ya afya ya mjamzito na mtoto tumboni. Pamoja na mlo kamili mjamzito hupewa virutubisho ziada (supplements) kwa ajili ya kuongeza madini kama ya chuma na Foliki. Mlo kamili unajumuisha vyakula vya
wanga, protini, mafuta, vitamini, madini na maji kama inavyochambuliwa hapa chini;
Nafaka na Vyakula vya Wanga.

Vyakula hivi huupa mwili nguvu za kufanya kazi ikiwemo ukuaji wa mtoto tumboni. Vyanzo vya wanga ni kama nafaka mbalimbali (mahindi, mtama, ulezi, mchele, uwele n.k), viazi, ndizi, mihogo. Ni vizuri mjamzito awe anapata nafaka kamili (whole grains) kama mahindi, ngano na mchele usiokobolewa.

Vyakula vya Protini.
Hivi ni muhimu kwenye kuujenga mwili, hasa kipindi cha mwezi wa 4 mpaka wa 9 ambacho viungo mbalimbali vya mtoto vinajengwa. Ni muhimu mama apate vyakula vya protini vya kutosha ili kuhakikisha ukuaji wa mtoto unaenda vizuri. Nyama za kuku, ng’ombe, mbuzi na wadudu waliwao kama senene, panzi; vyanzo vya protini za mimea kama maharage, soya, njugu, njegere, karanga, korosho n.k. Samaki, maziwa, mayai ni vyanzo vingine vya protini muhimu. Kwa wasiotumia vyakula vya nyama, unapotumia hivyo vyakula vya mbogamboga tumia kwa wingi kwanikiwango cha protini iliyo ndani ya mbogamboga ni chache ukilinganisha na iliyo ndani ya vyakula vya nyama.

Vyakula vya Mafuta.
Hutumika kwenye kuupatia mwili nguvu pamoja na ujengaji wa seli za mwili. Mara nyingi vyakula kama nyama, karanga, ufuta, alizeti, senene, panzi, samaki na matunda kama maparachichi huwa na mafuta. Ni vizuri kutumia mafuta yatokanayo na mimea ili kupunguza mafuta yenye lehemu (cholesterol) nyingi.


Mboga za Majani na Matunda.
Matunda na mboga za majani ni sehemu muhimu sana ya mlo wakati wa ujauzito, kwani huupatia mwili vitamini, madini na kambakamba kwa ajili ya kulainisha chakula. Vitamini husaidia kuimarisha kinga ya mwili sambamba na ufanyaji kazi wa mwili. Madini kama ya chuma, kalsiamu, zinki, madini joto (Iodine) na magneziamu ni muhimu kwa ukuaji salama wa mtoto tumboni mwa mama.
Madini ya chuma (Iron)
Mahitaji ya madini ya chuma nayo huwa makubwa kwa wajawazito. Madini hayo ni muhimu kwa utengenezaji wa damu ambayo huhitajika kwa wingi na mama pamoja na mtoto. Madini joto hupatikana kwa kula kwa wingi vyakula kama vile nyama, samaki, mayai, vyakula vilivyopikwa kwa nafaka zisizokobolewa (ugali wa dona, mkate mweusi, n.k) na mboga za majani kama vile spinachi na brokoli. Ili kupata madini hayo ya kutosha kutokana na vyakula hivyo, inashauriwa mjamzito kutumia pia vidonge vya Vitamin C (Vitamin C food supplements).
Vitamin B9 (Folic Acid)
Vitamini hii ni muhimu sana kwa mjamzito, ni kosa kubwa sana la kiafya kwa mjamzito kuwa na upungufu wa vitamin hii. Vitamin B9 ndiyo inayohusika na ukuzaji na uimarishaji wa mfumo wa fahamu wa kiumbe tumboni. Aidha, Vitamin hii ndiyo inayotoa kinga ili viungo vya mtoto visiathirike na kuepusha uzaaji wa watoto walemavu au wenye kasoro za viungo kama ‘midomo ya sungura’ na kadhalika.
Vyakula vyenye kiwango kikubwa cha Vitamin B9 ni pamoja na mboga za majani, juisi ya machungwa, mapeasi, vyakula vilivyopikwa kwa ngano na mchele (hasa brown rice) na mayai. Hata hivyo, kutokana na hali ya vyakula vyetu, mjamzito hawezi kupata kiwango kinachotakiwa cha vitamin hiyo kwa kula vyakula peke yake.

Ili kupata kiwango cha vitamin hiyo kinachotakiwa, mjamzito atatakiwa kutumia pamoja na vidonge vya lishe vya Vitamin B9 ili kuepuka upungufu huo. Inashauriwa kutumia vidonge hivyo miezi michache kabla ya kushika mimba na katika kipindi cha miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito, kipindi ambacho vitamin hiyo huhitajika kwa wingi.
Maji
Maji ni muhimu kwenye mmeng’enyo na unyonywaji wa chakula, pia husaidia kuzuia choo kigumu, mwili kuvimba na maambukizi ya mfumo wa mkojo (UTI). Inashauriwa mjamzito anywe maji si chini ya lita 2.2 kwa siku, yanaweza kuwa katika chai, juisi, au maji yenyewe. Ni vema zaidi kama akinywa maji kama maji zaidi na kupunguza vinywaji kama soda. Maji huchangia kwa asilimia 75 ya uzito wa mtoto wako atakapozaliwa. Usipopata maji ya kutosha utaishiwa na nguvu kwa asilimia 20 na kupata matatizo ya kukaukiwa (dehydration) na kichwa kuuma.

Mazoezi
Mazoezi ni muhimu kwa mama mjamzito ili kumpunguzia unene na kumfanya kuwa mwepesi wakati wa kujifungua, mama mjamzito asipofanya mazoezi aweza kunenepa na mwisho kumletea madhara, kama magojwa ya moyo hivyo kushindwa kujifungua vizuri. Acha fikira potofu kuwa ukipata ujauzito lazima umchukie mtu fulani au ushindwe kula baadhi ya vitu, ondoa hayo mawazo akilini mwako, kwasababu mimba si ugonjwa.
Pia waweza jenga akili ya mtoto wako tangu akiwa tumboni kwa kufanya mambo mazuri ambayo ungependa mwanao aje ayafanye atakapofika duniani. Usipendelee kunywa soda, kahawa, chai (mfano; chai bora), kulala lala na kuwa na mawazo.

2 comments:

  1. Asante sana kwa somo zuri,Je matumizi ya folic acid miezi mitatu ya kwanza ni vibaya.

    ReplyDelete

Powered by Blogger.