Umuhimu wa mazoezi kwa wajawazito
Miongozo mipya iliyotolewa nchini Marekani inapendekeza wanawake wajawazito kufanya mazoezi mepesi karibu siku zote za ujauzito. Tofauti na miaka 20 iliyopita, wataalamu sasa wanasema mazoezi humsaidia mama na mtoto.
Miaka 20 iliyopita, madaktari wangemuambia mama mjamzito kupumzika kadiri awezavyo, kwa kuhofia kuathiri ukuaji wa kiumbe aliye tumboni, na kusababisha uchungu wa mapema au hata mimba kutoka. Hata hivyo chuo cha wakunga na madaktari wa wanawake cha nchini Marekani ACOG, kinasema kujishughulisha kimwili kuna hatari ndogo sana na kunawasaidia wanawake wengi zaidi.
Miongozo ya hivi karibuni ya chuo cha ACOG, kuanzia mwishoni mwa mwaka 2015, ambayo inatazamwa kama alama teule duniani kote, inabainisha kuwa wasiwasi kuhusu uzazi wa njiti, kutoka kwa mimba au kudumaa kwa kijusi kutokana na mazoezi haujathibitishwa. Kwa mujibu wa ACOG, wanawake wanatakiwa kuhimizwa kushiriki katika mazoezi ya viungo na kuimarisha misuli kabla na baada ya ujauzito.
Mazoezi hayajali umri
Mazoezi shadidi ya kadiri ya kuanzia dakika kati ya 20 hadi 30 yanapendekezwa kwa siku nyingi za wiki kwa mwenye ujauzito usiyo na matatizo yoyote - wakiwemo wale walio na uzito uliopitiliza au wasio na shughuli za kutosha. Haijalishi pia wewe ni mtu wa umri gani.
Lililo jipya katika miongozo hii mipya ya Marekani ni kwamba inapendekeza wazi baadhi ya michezo, kama vile kuogelea au kutembea, ambayo ni rahisi kwa viungo, alisema mwanasayansi wa michezo Nina Ferrari kutoka kituo cha kinga wakati wa utoto na ujana katika mahojiano na DW.
Ferrari anajikita katika athari za mazoezi wakati wa ujauzito. Ferrari anasema jambo jipya ambalo hawakuwa nalo, ni kwa wajawazito waliokuwa wakimbiaji kabla ya ujauzito, ambao wameshauriwa kuendelea kukimbia hata wakiwa wana mimba pia.
Ferrari alisema ushadidi unaofanya nao kazi laazima ukuruhusu kufanya mazungumzo - ambayo wataalamu wanayaita mtihami wa kuzungumza. Hivyo ikiwa kwa mfano wewe siyo mkimbiaji, unaweza kuzingatia matembezi au kuogelea. Unaweza pia kubeba vitu vya uzito wa wastani katika kumbi za mazoezi, ilimradi tu usikae tu kwenye kochi lako kwa wiki 40.
Mazoezi pia yanaweza kukusaidia kuwa mwenye afya na kukuepushia kisukari cha ujauzito, ambacho kinaweza kukidhuru kiumbe tumboni na kinachohitaji mlo makhsusi, na katika wakati mwingine sindano za insulini hata kama kwa kawaida hauna ugonjwa wa kisukari. Kulingana na ACOG, mazoezi yanaweza pia kupunguza hatari ya tatizo linalosababishwa na kupanda kwa shinikizo la damu na vilevile kujifungua kwa njia ya upasuaji.
Faida za mazoezi
Wakati watafiti wakiendelea kutafuta njia za kuzuwia uzito uliopitiliza hasa miongoni mwa watoto wadogo, faida za mazoezi wakati wa ujauzito zimevutia usikivu, anasema Ferrari. Wakati hakuna ushahidi kuonyesha kuwa mtoto wako atakuwa na umbo la kimichezo kwa sababu umekuwa ukifanya mazoezi wakati wa ujauzito, mazoezi yanaweza kuathiri ukuaji wa viungo vya mtoto huyo, na hivyo kuwa na athari chanya katika utoto wake na kuendelea.
Ikiwa mazoezi laini ni zaidi ya kikombe chako cha chai, mazoezi yalioboreshwa ya yoga yanaweza kukusaidia kubakia mnyumbufu na kukusaidia pia dhidi ya maumivu ya mgongo - ambayo ni tatizo la kawaida wakati wa ujauzito, kwa sababu kina mama wanakuwa na kawaida ya kuumwa mgongo kutokana na uzito ulioongezeka.
Hivyo hakuna kisingizio - lakini unapaswa kuchagua mazoezi yako kwa umakini. Michezo ya kugusana kama vile soka, hoki, rugby au handiboli haitakikani. Pia jiepushe na michezo ya kuchupa majini, kupanda, kupanda juu ya zaidi ya mita 2,000, na jambo lolote linaloweza kutoa hatari ya kuanguka. Pia jihadhari sana wakati wa joto kali, na upumzike ukiwa na mafua, maumivu ya kichwa au unajiskia kizunguzungu.
No comments: