Header Ads

VYAKULA BORA 5 MUHIMU KWA MWILI WAKO


LISHE ni moja ya nguzo kubwa kwenye afya ya mtu, unachokula si tu kinafanya mwili unawiri na kuongeza nguvu pia kinaongeza ufanisi wa mwili katika kufanya shughuli zake kama usagaji wa chakula na usafirishaji wa chakula na takamwili.
Kama ulaji wako ni mbovu unaotegemea vyakula vilivyosindikwa na fast foods, ambavyo si tu vinakosa baadhi ya virutubisho muhimu bali pia vinakuja na sumu nyingi zikiwemo vionjo viongeza utamu (artificial sweeters) zitakazorudisha nyuma afya ya mwili wako.
Kinyume kabisa na vyakula asili ambavyo vitakupa vitamini za kutosha, madini, kukufanya ujisikie una nguvu muda wote kwa kukulinda dhidi ya magonjwa na hivo kufanya maisha yako kuwa ya furaha siku zote. Kuanzia sasa anza kula vyakula hivi:
NYANYA: Nyanya zina kemikali zinazoitwa flavonoids (anticarcinogenic) ambazo hupambana na visababisha saratani. Moja ya kemikali hiyo inaitwa lycopene ambayo hulipa tunda kama nyanya, tikiti ile rangi yake nyekundu. Lycopene ina nguvu kubwa katika kupambana na kuzuia saratani, hasa saratani ya tezi dume (prostate cancer).
Nyanya pia huchangia asilimia 38 ya vitamin C , 30% ya vitamini A na 18% ya vitamini K kwa matumizi ya kila siku. Kumbuka ili upate lycopene ya kutosha kwenye nyanya unahitaji kuzikaanga kidogo kwenye mafuta kisha ukala pamoja na mchanganyiko wako wa vyakula vingine ulivyoandaa.
BROCCOLI: Ni mboga ambayo ilitumiwa sana za Waroma hapo zamani. Mboga hii unaweza kuandaa kwa namna nyingi ikiwemo, kurosti, kula ikiwa mbichi, ni vizuri zaidi kutokana na kwamba upikaji unaharibu baadhi ya virutubisho.
Broccoli ina kiasi cha vitamini C mara mbili zaidi ya chungwa, madini mengi ya calcium kama maziwa na pia sifa ya kupigana na magonjwa kama saratani, kupambana na virusi, kutokana na wingi wa madini ya selenium.
Kikombe kimoja cha mtori wa broccoli kitakupa mahitaji yako ya siku nzima ya Vitamini C na Vitamini K na pia ni chanzo kizuri cha Vitamin A na potasium. Baadhi ya faida zingine zinazofahamika za broccoli ni hizi kupambana na saratani ama cancer, kupambana na mashambulizi ya magonjwa, kusaidia usagaji wa chakula na kuondoa sumu mwilini.
Faida nyingine ni ulinzi dhidi ya magonjwa mbalimbali hatari kama magonjwa ya moyo na kuwa na afya nzuri ya mifupa na meno.
TANGO: Ni moja ya tunda na mboga inayozalishwa kwa wingi zaidi duniani. Kuweza kutumia tango unaweza kukatakata na ukachanganya kwenye kachumbari yako, ama unaweza kutengeneza juisi kwa kutumia blenda yako ukiwa nyumbani.
Tango liliwahi kutumika kama dawa ya asili kwa ajili ya kutibu maumivu ya kichwa. Juisi ya tango husaidia kusafisha ngozi, na kuondoa uchovu kwenye macho. Maajabu haya ya tango yaliwafanya wanasayansi kuanza kutafiti juu ya tunda hili, zikiwemo mbegu zake.
Asilimia 90 ya tango ni maji ambapo vifuatavyo ni virutubisho vinavyopatikana: Vitamini K kwa ajili ya kuzuia maambukizi, Vitamini C kwa ajili ya kupambana na maambukizi, vitamini B ambayo huzalisha nguvu kwenye mwili na madini ya manganese kwa ajili ya kuimarisha mifupa.
Kwenye tango kuna madini ya potassium na magnesium kwa ajili ya afya ya moyo pia lina kemikali inayoitwa lignans ambayo hupatikana pia kwenye kabeji na vitunguu ambayo kazi ya lignans ni kupunguza hatari ya kuugua magonjwa ya moyo, pia muungano wa lignin na bakteria wazuri walioko kwenye mfumo wa usagaji chakula husaidia kupunguza hatari ya kuugua badhi ya saratani kama saratani ya matiti, kizazi, na saratani ya tezi dume.
PARACHICHI: Ukilinganisha na matunda mengine, tunda hili lina virutubisho vingi zaidi na hutakiwi kulikosa kwenye mlo wako kila siku kwani lina virutubisho vifuatavyo: Vitamini K ambayo inaweza kuchangia asilimia 36 ya mahitaji yako mwilini, asilimia 30 ya mahitaji yako ya siku ya vitamini B.
Muhimu zaidi ni kwamba parachichi ni moja ya matunda machache ambayo yana kiasi kikubwa cha mafuta mazuri (god fats) hivyo kupunguza hatari ya kuugua magonjwa ya moyo na uzito mkubwa.
NAZI: Mafuta ya nazi ambayo hutengenezwa kutoka kwenye nazi iliyokomaa hutumika zaidi katika nchi za wenzetu kama India, Sri lanka, Thailand na Ufilipino ambako mmea huu hulimwa kwa wingi zaidi, hapa nchini pia mmea huu hulimwa sana mikoa ya Pwani kama Tanga, Pwani, Dar es Salaam na Mtwara.
Mafuta ya kula ya nazi yanaweza kutumika katika mapishi ya vyakula, kuchanganywa kwenye saladi, ama unaweza kutumia kutengenezea juisi.
Kwa wale ambao wanapunguza uzito basi badala ya kutumia wanga na sukari, anza kutumia nazi kama chanzo cha mafuta mazuri (medium chain fats) ambazo huweza kuvunjwa vunjwa kirahisi ndani ya mwili na hivyo kuweza kubadilishwa na ini kuwa nguvu moja kwa moja pasipo kuhifadhiwa kama mafuta kama ilivyo ukila wanga na sukari.
Nazi ina uwezo mkubwa wa kupambana na bakteria, virusi na protozoa. Matumizi ya nazi pia yatakusaidia kuimarisha afya ya moyo, kusapoti ufanyaji kazi wa tezi ya thairodi, kuimarisha utendaji kazi wa ubongo, kuimarisha kinga ya mwili.
Nazi pia ni chanzo kizuri cha kutoa nguvu na kusaidia kuimarisha utendaji kazi wa mwili katika kukuwezesha kupunguza uzito.

No comments:

Powered by Blogger.